Wiki iliyopita, Laiton Mtafya alisimulia namna alivyojiingiza kwenye kundi la majambazi akiwa na lengo la kupata utajiri. Hata hivyo, harakati zake hizo zilimsababisha anusurike kifo baada ya kupigwa na kumwagiwa maji ya betri machoni huku mwenzao mmoja akipasuliwa jicho na wananchi wenye hasira.
Leo anaanza kwa kusimulia namna alivyokuwa akimshawishi daktari katika hospitali aliyokuwa amelazwa amruhusu kutoka wodini, wakati ndugu zake wanataka aendelee kupatiwa matibabu. Sasa endelea…
“Basi nilipoona imeshindikana kwa dokta nilirudi kwenye chumba changu wodini, kesho yake asubuhi dokta alinikuta nimekaa mlangoni pake namngojea. Alipofika tu, anaingia ndani na mimi naingia.
“Aliniuliza inakuwaje, nilikasirika nikamjibu vibaya, akaniuliza kwa nini unakuwa na hasira? nikamwambia ulikuwa unataka nilale uniongezee gharama? Akaniambia ‘hapana ndugu zako waliniambia inawezekana wewe umechanganyikiwa’.
“Nikamwambia inawezekana wewe ndiyo umechanganyikiwa, kama niliweza kutoka eneo la tukio, nikaenda polisi na kuja hospitali halafu unasema nimechanganyikiwa, akasema ndugu zangu walisema nilale pale kwa siku moja zaidi.
“Basi, nikaandikiwa bili yangu, nikatoka pale nikaenda kuwaona wenzangu (katika hospitali nyingine) walikuwa kwenye hali mbaya sana. Naongea nao lakini hawaoni, wote wawili halafu yule mmoja alikuwa amevimba sana.Yule aliyekwenda kubebwa kule saa nane mchana.
“Niliwapa pole nikarudi. Baada ya siku sita yule mmoja aliruhusiwa, lakini aliyepasuliwa jicho alikaa hospitali mwezi mzima.
Aapa kuendelea na wizi hadi atajirike
“Baada ya kutoka hospitali tulikutana wote watatu tujadili kitu gani cha kufanya. Tulikubaliana kila mtu aseme anafikiri nini kuhusu tukio lililotukuta. Alianza mdogo wangu kuzungumza, alisema ‘kuanzia sasa katika maisha yangu siibi tena na hapa kijijini naondoka, ninakokwenda siwezi kusema ila hapa ninaondoka.
“Alifuata aliyetobolewa jicho, alisema; ‘siibi tena katika maisha yangu, ila nitarudi kwenye kile kijiji, kitu nitakachofanya hakuna mtu atakayekuja kuamini’. Tukamuuliza utafanya nini? Akasema’ nitakwenda pale usiku, wanikamate, wasinikamate, kama kuniua waniue, nitakwenda kuchoma moto kijiji chote,’ alisema lakini hakufanya hivyo kwa sababu alikufa kwa maradhi.
“Nikafuata mimi, nikasema katika maisha yangu sitaacha wizi mpaka nitajirike, la sivyo nife, lakini wizi mimi siachi. Basi tukapeana mikono pale kila mtu akaendelea na maisha yake.”
Anasema baada ya makubaliano hayo, wenzake walihama kijijini pale, huku yeye akibaki na mwenzake mmoja ambaye hakwenda kushiriki wizi siku ile kwa kuwa alikuwa amelewa.
Anusurika kupigwa risasi kichwani
“Mimi na yule ambaye hakwenda kwenye lile tukio tukatafuta vijana wengine wanne; wawili kutoka Igurusi na wawili kutoka Tukuyu. Baada ya hapo tukaenda kufanya tukio lingine la wizi Tukuyu mjini.
“Siku hiyo hatukuwa tumekwenda kwa ajili ya kuvunja, kwa sababu tulikuwa tunatumia funguo za ‘master key’. Nimefungua kufuli la kwanza kwenye duka moja hivi, kile kitendo tu cha kuinama nilipishana na risasi, ikapiga juu. Niliona giza, yule aliyepiga risasi angekuwa makini apige risasi ya pili angenipiga.
“Kwa sababu kuondoka pale nilishindwa nilikuwa sioni, zile cheche za risasi ziliniwekea vialama fulani hivi. Basi nikatoka pale wenzangu wameshakimbia, tumesambaratika.
“Aliyepiga risasi hakujulikana yuko wapi, kile kitendo mimi sikukubali nikasimama nikasema aliyepiga alikuwa wapi na kwa nini wenzangu hawakumwona. Baada ya kuchunguza nikaona kuwa alikuwa chini ya meza.
“Wenzangu walikuwa wameondoka, lakini kwa sababu eneo la kwenda kukutana nilikuwa nalifahamu, basi nikaenda nikawakuta wenzangu. Tukaanza kumlaumu mtu aliyepewa kazi ya kuchora ramani kuwa alichora kizembe sana.
“Ramani ndiyo inayotuongoza tufanikiwe, ukikosea kwenye ramani, kwenye tukio lazima mkamatwe. Mkichora ramani vizuri hamuwezi kukamatwa. Mtu anayechora anaweza kukaa mahali siku nzima, akalala hapo ili aangalie walinzi wanakaa wapi.
“Anaweza kukaa sehemu labda kwenye ‘grocery’ anakunywa bia yake huku anachunguza mazingira bila ya watu wa pale kuelewa. Huko ndiko kunaitwa kuchora ramani.
“Ramani nyingine zinachorwa kutokana na mtu labda kesho atasafirisha fedha kiasi fulani. Mchoraji wa ramani ndiyo mtu mwenye kazi ngumu kuliko mtu mwingine yeyote.
“Basi tukamlaumu, baadaye akaomba msamaha kwamba alichora ramani vizuri ila ilikuwa bahati mbaya. Baada ya hapo tulikwenda sehemu nyingine kuiba mabelo ya nguo. Tulivunja tukaiba mabelo manne, lakini tulikuja kukamatwa wakati wa kuuza. Tulikuwa tumechukua nguo kidogo kama ‘sample’ kwenda kumwonyesha mteja, alipoziona alitaka apelekewe mzigo.
“Mimi sikuwa nimekwenda, nilikuwa eneo la mzigo nasubiri aliyekwenda kupeleka sample. Alipoondoka kuja kuchukua mzigo, yule mteja alimpigia simu mwenye mzigo aliyeibiwa, alikuwa ametoa taarifa kwenye maduka yote.
“Bila taarifa yoyote, akaja, nikamuuliza amesemaje, ‘nimeambiwa nipeleke mzigo’ nikamuuliza umekwenda kwa nani? akataja. Nikamwambia huo ni mtego hizo nguo usipeleke. Hata huu mzigo hapa tuuhamishe.
“Hakwenda yeye kule dukani, akaenda mtu mwingine, kama nilivyokuwa nimeota ikatokea hivyohivyo, alipofika tu pale na mwenye mzigo alikuwa amefika. Katika purukushani za kutaka kumkamata yule kijana akawa mbishi tajiri akapiga risasi juu.
“Ilipopigwa risasi akatokea mjomba wa yule kijana akauliza kuna nini? wakati anataka kumsaidia mjomba wake, alipigwa risasi ya mguuni. Alianguka chini kila akitaka kuinuka anaanguka chini. Yule kijana alifikishwa polisi akiwa na sample sita za nguo, vishati vya watoto na kaptura.
“Alipoulizwa hizi nguo vipi, alisema kuwa alikuwa amemnunulia mtoto wake anayeishi Dar es Salaam, ila anataka auze apate hela za matumizi.
“Huku nyuma kumbe wakati tunahamisha mzigo kuna watu walituona, tukakamatwa watu wawili, lakini mzigo haukukamatwa kwa sababu mwenzetu mmoja aliusafirisha.
“Ile kesi ilitusumbua, mimi niliwekewa dhamana, lakini wenzangu waliwekwa ndani. Baadaye wanakijiji waliandamana ikaonekana polisi wa eneo lile wanamsaidia yule tajiri aliyempiga mtu risasi ya mguuni.
“Kwa hiyo tajiri naye akakamatwa akawekwa ndani kwa makosa ya kutumia risasi kinyume cha sheria. Kwa kuwa yule tajiri alikuwa ana kesi nyingine, hakuweza kufika mahakamani, kesi yetu ikaonekana haina nguvu.
“Yule mwenzetu ambaye alikimbia na mabelo ya nguo, alirudi lakini hakuwa na hela, nikamfokea akaamua kwenda kujiunga na kikundi kingine cha wezi kule Njombe, lakini bahati tukio la kwanza tu aliuawa akatupwa kwenye mto.
“Nikabakiwa na vijana watatu, nikaona hawatoshi. Kabla sijaongeza vijana wengine nilifuatwa na vijana wengine kutoka Njombe waliniambia wananitaka tukafanye kazi fulani. Huwa tunakuwa na mawasiliano, unajua mtu ukiwa msumbufu watu wanakufahamu.
“Pia mnajuana vizuri sana mnapokuwa kwenye magereza, mnaulizana wewe unatokea wapi? Iringa, mimi Dar es Salaam. Tupeane anuani, nikitoka hapa tutakutana sehemu gani, anakwambia.
“Basi tukatoka na wale vijana hadi Njombe. Tulivyofika, tukio la kwanza tu walinzi walitushtukia wakati tunavunja, ila mimi sikuwa mlangoni nilikuwa ninawalinda wenzangu. Tulipokurupushwa mimi sikuwa mwenyeji Njombe, tukio lilitokea eneo linaitwa Ramadhan.
“Wakati tunakimbia bahati mbaya mimi niliingia kwenye korongo nikaanguka wakanikamata, wakaanza kunipiga sikupoteza fahamu, lakini walinivunja mguu hapa chini (anaonyesha).
“Baada ya kunivunja mguu wakakimbia, halafu wakaanza kusogea raia wengine mmoja mmoja. Wakasema wanisaidie wakanikokota hadi Hospitali ya Kibena Njombe. Nikalazwa pale kama wiki tatu.
“Wakati nipo hospitali, kuna kesi ambayo nilikuwa nje kwa dhamana, walipoona sionekani wakanifutia dhamana. Nimetoka hospitali nikiwa bado nina PoP mguuni, nilipofika nyumbani nikakamatwa tena
ITAENDELEA!
MWANANCHI.
1 comment:
aziz bilal02:36
1
Reply
kwetu kunatisha sana ka mambo yenyewe ndiyo haya ni afadhali tuendelee kuishi ktk nchi za wenzetu milele.
Post a Comment