Friday, 5 September 2014

POLISI TUNAUSAKA MTANDAO WA MAUAJI YA ALBINO



JESHI la Polisi nchini, linaendelea na oparesheni kali yenye lengo la kuunasa mtandao mzima unaojihusisha na matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ili waweze kukamatwa, kufikishwa mahakamani wakiwemo waganga wa jadi.




Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Isaya Mngullu, alisema hivi karibuni yameibuka matukio ya kuwaua na kuwajeruhi watu wenye ulemavu wa ngozi kwa visingizio vya imani za kishirikina.



"Matukio haya ni mabaya, yanahitaji kulaaniwa na kukemewa na kila mmoja wetu ndani ya jamii... kipindi cha nyuma yalikuwepo tukaweza kuyadhibiti kwa kiwango kikubwa tukishirikiana na jamii ambayo ilitupa taarifa ambazo zilisaidia kukamatwa kwa watu waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivi," alisema.


Alisema mwaka huu, matukio matatu ya kuwaua na kuwajeruhi watu wenye ulemavu wa ngozi, yamejitokeza tena ambapo tukio la kwanza lilitokea Mei 12 mwaka huu, Mjini Bariadi, mkoani Simiyu ambapo Munghu Lugata, aliuawa na baadhi ya viungo vyake kuchukuliwa.


Aliongeza kuwa, katika tukio hilo watuhumiwa watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo tukio jingine lilitokea Agosti 5 mwaka huu, katika Wilaya ya Kariua, mkoani Tabora ambapo Pendo Sengerema, alikatwa mkono wake wa kulia na watuhumiwa watatu wamekamatwa.


"Tukio la tatu lililotokea Agosti 16 mwaka huu, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mungu Masanga akiwa amelala nyumbani na mumewe, Mapambo Mashili, walivamiwa na watu wasiofahamika wakamkata kiwiko cha mkono wa kushoto.


"Mumewe ambaye alijaribu kupambana na watu hao ili wasiweze kutekeleza uhalifu huo, aliuawa na watuhumiwa watatu tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani," alisema.


Mngullu alisema jeshi hilo linaendelea na msako mkali wa kuwasaka na kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wakiwemo waganga wa jadi wanaoshirikiana na watuhumiwa.


Alitoa onyo kwa yeyote anayeendelea kuchochea matukio hayo wakiwemo waganga wa kienyeji na wapiga lamri, kuacha mara moja badala yake wafanye kazi halali za kuwaingizia vipato ili waweze kuendesha maisha yao si vinginevyo.

 Chanzo;Majira

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!