Tuesday, 9 September 2014
MASHINE ZA KISASA ZA EBOLA ZAFUNGWA
KATIKA jitihada za Serikali kuimarisha mifumo ya kukinga taifa na maambukizi ya virusi hatari vya homa ya ebola, mashine mpya sita za kisasa zaidi za kukagua wageni wote wanaofika nchini kupitia usafiri wa anga, zimewasili nchini na tayari zimefungwa katika viwanja vikubwa vya ndege.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani, alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Ghala Kuu la Dawa la Taifa, Keko jijini Dar es Salaam.
“Ununuzi wa mashine hizi ni ushahidi dhahiri kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana kuikinga nchi na balaa hili la ugonjwa hatari wa ebola, ambao kama ambavyo mnajua kwa sasa umeleta maafa makubwa kwa wenzetu huko Afrika Magharibi. “Mashine hizi zina uwezo mkubwa wa kupiga picha ya mwili mzima wa mtu na kutoa taarifa kwa maofisa wanaohusika, kuhusu uhalisia wa afya yake na hasa uwepo au kutokuwepo kwa virusi vya ebola katika mwili wake,” alifafanua Mwaifwani.
Za zamani
Mashine hizo kwa mujibu wa Mwaifwani, ni tofauti na zilizokuwepo awali, ambazo zilikuwa za mkono na za sasa abiria watapita katika mashine hiyo na washukiwa kubainika.
Mwaifwani alisema mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali iliingiza nchini dawa za msingi na vifaa tiba vya kumhudumia mgonjwa wa ebola vya kutosha.
Mbali na dawa hizo, pia iliingiza mashine za kushika kwa mkono, kwa ajili ya kuwakagua wasafiri wote wanaoingia katika viwanja vya ndege vya kimataifa, ambazo zilikuwa zikitumika kabla ya mashine kubwa kuwasili nchini.
Alitaja viwanja ambavyo mashine hizo zimefungwa kuwa ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, ambako kumefungwa mashine tatu, huku viwanja vya ndege vya kimataifa vya Mwanza, Zanzibar na Kilimanjaro, vikipewa mashine moja kila kimoja.
Kwingineko
Kuhusu maeneo mengine ya mipaka ya ardhini na majini, Mwaifwani alisema ununuzi wa mashine hizo ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuwakinga wananchi na ugonjwa huo, kwa kuwapima kwa ufanisi watu wote wanaoingia nchini kutoka nchi za nje.
Alisema muda si mrefu, mashine zaidi zitanunuliwa na kuwekwa katika mipaka rasmi ya ardhini na majini.
“Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwa Serikali ipo makini sana na ugonjwa huu hatari ambao umeua zaidi ya watu 1,900 wakiwemo maofisa tabibu na afya 380 huko Liberia, Senegal, Sierra Leone, Guinea, Conakry, Nigeria na hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC),” alisema.
Mwaifwani aliwaomba wananchi nchini kote, kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama, pale wanapoona mtu anapita katika ‘njia za panya’ katika mipaka yetu au mtu mwenye dalili za ebola, ili kuepusha nchi na maafa yanayoweza kuzuilika.
“Ingawa tumeleta mashine hizi za kuwakagua wasafiri, lakini si wageni wote watapita katika viwanja vya ndege, wengine tuna uhakika wanapita njia za panya, sasa ni jukumu letu sote kupambana ili kunusuru Taifa letu na ugonjwa huu hatari ambao haujapata tiba,” alisisitiza Mwaifwani.
Ugonjwa huo uligunduliwa mwaka 1976 katika nchi za Sudan na DRC na kupewa jina ebola, linalotokana na Mto Ebola uliopo DRC. Jina hilo ndilo linalotumika hadi sasa kutambulisha ugonjwa huo kimataifa.
Taarifa za kitafiti zinaonesha virusi vya ugonjwa huo, vinabebwa na wanyama wa mwituni, hasa sokwe mtu na wanyama jamii ya nyani, ambao ni kitoweo maarufu DRC na nchi za Afrika Magharibi, ambazo nyingi zina misitu minene, ambayo inazuia ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo, ambao ni kitoweo bora na salama.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa sasa kuna wagonjwa wa ebola 3,500 katika nchi za Liberia, Sierra Leone, Guinea, Nigeria, Senegal na DRC.
Wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza na Taifa kupitia mkutano wake na wazee wa Mkoa wa Dodoma, alisema Serikali imejipanga vizuri kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini.
HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment