WANAFUNZI 808,111 wa Darasa la Saba kesho wanaanza mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utakaofanyika kwa siku mbili mfululizo.
Akizungumza jana Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bharalusesa alisema idadi hiyo ni kwa wanafunzi wote wanaofanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Miongoni mwa hao, 783,223 ni wanaofanya kwa Kiswahili na waliobaki ni kwa Kiingereza Mwaka jana, wanafunzi wapatao 868,030 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.
Kwa idadi hiyo ya watahiniwa wa mwaka huu, kunafanya idadi ya watahiniwa kupungua kwa zaidi ya wanafunzi 59,000. Kwa mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa la saba, jumla ya alama zote ni 250 ambazo hugawanywa katika madaraja matano yaani A mpaka E.
Mchanganuo uko hivi: Daraja A huanzia alama 201 hadi 250, B inaanzia 151 hadi 200.
Daraja C ni 101 hadi 150 na D inaanzia 51 hadi 100. Chini ya alama 50 ni daraja E. Watoto hawa watakuwa zao la pili tangu Serikali izindue Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN).
Akizungumzia maandalizi ya mtihani huo, Bharalusesa alisema: “Maandalizi yamekamilika, usambazaji wa mitihani na vifaa vingine pia umeshakamilika, hii ni mitihani ina unyeti wake siwezi kusema iko wapi.”
Aidha, Bhralusesa alisema katika malengo ya BRN, wizara yake ilipanga mwaka huu kiwango cha ufaulu kiongezeke hadi kufikia asilimia 70.
Katika mtihani wa mwaka jana, ufaulu ulikuwa ni asilimia 50.51 ikiwa ni ongezeko la ufaulu kwa asilimia 19.89 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2012 ambao ulikuwa ni asilimia 30.72.
HABARI LEO
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment