Kama ilivyo ada kila msimu kunakuwa na damu changa inayoonekana kusisimua watazamaji. Vilevile kuwarithi waliotangulia. Je unafahamu ni wachezaji gani chipukizi wanaoonekana kuwa tishio kutoka barani Afrika? Hawa ndio wa kuwatupia macho:
Yacine Brahimi
Miaka kumi na tisa baada ya Rabah Madjer kuisaidia klabu ya Porto kufika mbali kwenye ligi ya mabingwa Ulaya, klabu hiyo yenye mafanikio zaidi nchini Ureno imemsajili kiungo mshambuliaji mwingine kutoka nchini Algeria- Yacine Brahimi.
Mhitimu huyo wa Chuo cha Clairefontaine amerithi jezi namba 8 ya Madjer hivi sasa yuko tayari kuonyesha maajabu ndani ya Ureno. Akiwa Granada, Brahimi alikuwa mchezaji mwenye chenga nyingi akicheza winga wa kushoto hivyo inawezakana akaitumikia klabu yake mpya kwa nguvu ile ile.
Abdelaziz Barrada
Watu wengi katika soka duniani wanajiuliza maswali mengi kuhusiana na uamuzi wa Abdelaziz Barrada kuikacha klabu yake ya Emirati ya Al Jazira aliyojiunga nayo mwaka jana.
Lakini hivi sasa kiungo huyu amesaini mkataba mpya na timu ya Olympique de Marseille ya Ufaransa kwa Euro 10 milioni.
Akiwa kamili kila idara, Barrada raia wa Morocco ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Sifa yake kubwa ni kupiga mashuti mazito na pasi za uhakika. Akiwa ni zao la kituo cha soka cha timu ya Paris Saint-Germain, Barrada mwenye miaka 25 anatarajiwa kuonyesha kipaji cha kipekee kutoka Afrika.
Sadio Mane
Ni kama bahati ya mtende vile kwa Red Bull Salzburg kubaki na kinda hili. Sadio Mané (22)mshambuliaji wa Kisenegali aliwahi kuwaniwa na Leverkusen, Dortmund na Hoffenheim, lakini klabu hizo hazikufanikiwa kumnasa kutokana na ukweli kuwa klabu yake ilihitaji kiasi cha Euro 20 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Rekodi aliyo nayo katika upachikaji wa mabao inamuweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika soka.
Riyad Mahrez
Hakuna aliyetarajia kama Riyad Mahrez atafanya alichofanya baada ya kusaini mkataba na Leicester City mwezi Januari. Mchezaji huyu wa kimataifa kutoka nchini Algeria amekuwa kivutio kikubwa miongoni mwa mashabiki wa soka.
Hivi sasa mchezaji huyu ni miongoni mwa wachezaji wazuri zaidi ndani ya Leicester. Uchezaji wake unafananishwa kwa karibu kabisa na Angel Di Maria wa Manchester United.
Bertrand Traore
Kipaji chake kilijulikana tangu akiwa na umri wa miaka 16. Akiwa na miaka 18 Bertrand Traore kutoka Burkina Faso alisaini kuichezea timu ya Chelsea. Hivi sasa yupo Uholanzi akiichezea klabu ya Vitesse kwa mkopo kutoka Chelsea.
Kwa kumfuatilia kupitia mechi zake za Ligi Kuu utaweza kushuhudia ni jinsi gani ana uwezo wa kusakata kabumbu.
Ramy Rabia
Sporting Club de Portugal ni moja kati ya klabu maarufu nchini Ureno iliyowekeza kwa mchezaji Ramy Rabia kutoka Misri. Ramy Rabia ni miongoni mwa wachezaji nyota wa Misri. Rabia (21) ambaye ni mlinzi wa kati ni zao la chuo cha mafunzo ya mpira cha Al Ahly.
Cheikhou Kouyate
Miaka minane baada ya kuishi nchini Ubelgiji , Cheikhou Kouyate hatimaye amekamilisha ndoto yake ya kuchezea Ligi Kuu England. Mchezaji huyu wa Kisenegali ni kivutio kikubwa kwa timu yake ya West Ham United.
Aymen Abdennour
Aymen Abdennour alitumia muda mwingi akiwa na Tolouse kabla ya kwenda ligi 1. Mchezaji huyu hivi sasa anachezea timu ya Monaco ya nchini Ufaransa na ni miongoni mwa wachezaji tegemeo.
Abdennour amedhamiria kuonyesha kuwa yeye ni mlinzi bora mwaka huu.
Imetafsiriwa na Maimuna Kubegeya.
No comments:
Post a Comment