Saturday, 20 September 2014
KINANA AMWAGIA SIFA MAMA SALMA KIKWETE
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amempongeza Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mama Salma Kikwete kwa juhudi za kusaidia na kuinua wanawake.
Akizungumza na wanafuzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya WAMA-Nakayama iliyopo Kijiji cha Nyamisati wilayani Rufiji baada ya kusimama kwa muda katika shule hiyo, Kinana alisema Mama Kikwete ni mtu shupavu mwenye kujali kusaidia na kuwainua wanawake na watoto wa kike.
Alisema juhudi zake ni za kupongezwa. Alisema amekuwa akijituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto wa kike na wanawake kwa lengo la kuwakomboa.
“Shughuli za kijamii zinazofanywa na Mama Salma ni za kupongezwa na jamii nzima, anasaidia watu bila ubaguzi na ndio maana anasaidia wasichana kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.”
Mkuu wa Shule hiyo, Suma Mensah, alisema shule hiyo imekuwa akipokea wanafunzi wasio na uwezo, yatima kutoka sehemu mbalimbali nchini, waliofaulu ambao hawana uwezo wa kujiendeleza kimasomo.
Alisema wanapata faraja kuona watoto hao wanaishi kwa amani na upendo na kuwa na furaha kiasi cha kusahau hali mbaya ya familia zao au kufiwa na wazazi, hali ambayo inawapa walimu moyo wa kufundisha kwa bidii.
“Wakiwa hapa shuleni wanalelewa vizuri kiasi kwamba hawakumbuki familia zao na hata wakati wa likizo wengine huomba kubaki shuleni, jambo hili linatupa faraja na kuona wanafunzi wana amani na wanakipata kile ambacho wanatakiwa kukipata,” alisema.
Aidha alisema juhudi za Mama Salma zimeweza kufanikiwa kwani watoto ambao hawakuwa na uelekeo wa maisha, wengi walikuwa wakiishia kuolewa kutokana na ugumu wa maisha sasa wamepata msaada.
Shule hiyo inatoa elimu ya sekondari kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Sita ikiwa na takribani wanafunzi 360. Kwa mara ya kwanza mwaka jana, wanafunzi 68 walifanya mtihani wa Kidato cha Nne mtihani wa taifa na hakuna aliyefeli.
Katika matokeo hayo wanafunzi 10 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 20 walipata daraja la pili na wanafunzi 19 walipata daraja la tatu na wale wa daraja la nne ni 19.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment