WATOTO watatu wa familia moja, wakazi wa Nyankumbu, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana baada ya nyumba yao kuteketezwa kwa moto uliowashwa kwa mafuta ya petroli na mtu asiyefahamika.
Dada mkubwa wa marehemu hao ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari Mwatulole na wazazi wao, walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo ambalo chanzo chake ni ugomvi wa ardhi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya hiyo, Dkt. Adam Sijaona, alisema miili ya watoto hao imehifadhiwa hospitalini hapo.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Reginald Robert (9), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Nyankumbu Mkombozi, Sophia Robert (6) aliyekuwa akisoma darasa la kwanza shuleni hapo na Remijius Robert (4).
Majeruhi ni Scholastica Robert (15), ambaye amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Wazazi wa watoto hao ambao pia walijeruhiwa katika tukio hilo ni Bi. Angelina Gaspa (36), ambaye amelazwa hospitalini hapo akiwa na majeraha katika mkono wake wa kulia, mgongoni, begani pamoja na Bw.Robert Remijius (45) aliyejeruhiwa kichwani.
Akizungumza kwa tabu akiwa wodini, Bi. Gaspa alisema siku ya tukio walikuwa wamelala watoto wakiwa chumbani kwao ambapo ghafla alisikia watoto wakipiga kelele na kusema ‘mama tunakufa’ na alipokwenda kuwaangalia, akakuta nyumba inateketea kwa moto.
“Nilikuta nyumba nzima ikiwaka moto, tulipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walifika na kuanza kuvunja milango pamoja na ukuta ili waweze kutuokoa.
“Mimi na mume wangu tulijitahidi kuvunja tofali japo tupate sehemu ya kupita na majirani walipofanikiwa kuvunja nyumba, tayari watoto wangu watatu walikuwa wameteketea kwa moto,” alisema.
Aliongeza kuwa, anaamini chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa ardhi uliokuwepo kati yao na mkazi mmoja wa eneo hilo (jina limehifadhiwa) ambaye alifika na kuchimba kisima katika eneo ambalo wao walilinunua kisheria lakini alidai ni lake.
“Tunaishi vizuri na majirani zetu, yote tunamuachia Mungu kwani hata tulipotaka kumlipa ili aondoke katika eneo letu alikataa na mgogoro huu umedumu kwa mwaka mmoja,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Manzie Mangochie, alisema kitendo hicho cha kikatili hakitavumilika na aliyefanya tukio hilo lazima asakwe kwa nguvu zote ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria mara moja.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kalangalala, Bw. Hamad Hussein, alisema watu waliofanya ukatili huo walitumia mafuta ya petroli kuyamwaga mlangoni mwa nyumba hiyo na kusambaa vyumbani ukianzi katika chumba walicholala watoto hao.
“Katika eneo la tukio, tumekuta ndoo ya plastiki yenye ujazo wa lita tano iliyotumika kuhifadhia mafuta hayo, tunaomba ushirikiano kwa wananchi ili tuwatie mbaroni wote waliohusika,” alisema
No comments:
Post a Comment