Wanafunzi wa darasa la awali Shule ya Msingi Nakayaya wakiwa darasani. Hata hivyo shule hii haina chumba cha darasa la awali chumba hiki kimejengwa kwa matumizi mengine na kwa sasa kinatumika kwa muda kwa kuwa kipo katika ujenzi.
Mwalimu Christina Komba (kulia) wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko akiwa darasani.Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani) ofisini kwake. Mwalimu wa muda wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi akionesha baadhi ya nakala za vitabu walivyonavyo.
Tunduru
SHULE nyingi za msingi zenye madarasa ya awali Wilayani Tunduru zimekuwa zikiendeshwa kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na vitabu vya baadhi ya masomo kabisa huku zikiwa na upungufu mkubwa wa vitabu kwa masomo mengine.
Hali hiyo imebainika hivi karibuni katika uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya Shule za Msingi za Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma huku walimu wa madarasa hayo wakielezea jitihada binafsi wanazozifanya kukabiliana na changamoto hiyo.
Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko akizungumzia hali hiyo alisema darasa lake halina vitabu vya masomo kama ya sanaa, Haiba na Michezo na wala miongozo ya namna ya ufundishaji hivyo kila mwalimu anayefundisha darasa hilo hubuni nini afundishe katika masomo hayo.
“Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa tunaazima au ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa hata ukienda madukani katika Wilaya yetu vitabu kama Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani," alisema Bi. Komba.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela akizungumzia shule yake alisema licha ya usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka upatikanaji wa bajeti ya kuendesha elimu hiyo ni changamoto kubwa huku uchangiaji kwa wazazi ikiwa wa kusuasua.
“…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, nyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna hata madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa darasa hili,” alisema Mkwela.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali alisema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua kutokana na kutokuwa na bajeti inayoletwa kusaidia elimu hiyo, isipokuwa kwa baadhi ya mwaka kuletwa madawati kumi kwa ajili ya wanafunzi wa awali.
“…Uendeshaji elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali.
Kwa upande wake mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi akitolea mfano shuleni hapo alisema vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja moja tu kwa kila somo, ambazo huzitumia yeye mwenyewe.
Aidha mwalimu Milanzi aliongeza kuwa darasa hilo licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni kila mara halimo jambo ambalo husababisha hali kuendelea kuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo, Hadija Makamla alisema anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo, nakala ambazo pia ni chache ukilinganisha na ukubwa wa darasa lake. “…Ninazo nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
2 comments:
aziz bilal13:56
1
Sophy kifanyike nini ili hawa watoto waweze kupatiwa msaada?inasikitisha sana
ndio hivyo inasikitisha kuona mpaka leo bado kuna watoto wanasoma katika mazingira kama haya..
Post a Comment