Friday 26 September 2014

ASKOFU: WATANZANIA WATACHUKUA URAIA KWINGINE"


ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini amesema kukataa uraia pacha ni sawa na kukubali kupoteza watoto na nchi kubaki kama kisiwa wakati nchi nyingine zinafanya hivyo, jambo ambalo Watanzania wengi watakimbilia uraia wa nchi nyingine.



Alisema watafanya hivyo kwa lengo la kupata kazi, ikiwa ni pamoja na kupoteza wanamichezo ambao wanaenda nje ya nchi kwa ajili ya masilahi.
“Mimi naona hili lingeruhusiwa bali kuwa masharti ya kutogombea nafasi yoyote ya uongozi ni vema tukaangalia nchi kama Marekani wanavyonufaika na suala hilo,” alisema.
Akizungumzia suala la Zanzibar kuruhusiwa kujiunga na mashirika ya kimataifa, alisema hakubaliani nalo, kwani suala hilo linafanya kusiwe na maana ya Muungano.
Alisema haiwezekani kusema Zanzibar, si nchi wakati inakuwa na sera mbili ya kujiamulia mambo yake na yale ya muungano, jambo ambalo ni hatari kwa ajili ya usalama wa nchi. Haki za binadamu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba alisema hajaridhishwa na mchakato mzima wa Katiba hadi sasa.
Pia, alisema Rasimu hiyo mpya haijagusa eneo la haki za binadamu. Alisema katika Rasimu zote za awali ya kwanza na ya pili, zilibainisha kipengele kinachoelezea mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu kuibana dola ili iweze kutekeleza haki za binadamu.
“Lakini nashangaa katika rasimu hii mpya kipengele kilichopo Ibara ya 53 (3) inaelezea juu juu tu suala la haki za binadamu bila kuitaka mikataba hii kama sisi wadau na wananchi tulivyochangia, hii haina maana kabisa,” alisema Bisimba.
Mawaziri kuwa Wabunge Katika eneo hili, Askofu Kilaini alisema rasimu hiyo ya BMK ina vipengele vingi ambayo anaamini kuwa wananchi watavikataa ikiwa ni pamoja na yeye kama mawaziri kuwa wabunge na kutoruhusu wananchi kuwaondoa wabunge ambao hawawaridhishi.
Alisema kipengele hicho ingefaa mawaziri kuwa na kazi moja tu ya utendaji Serikalini na kueleweka hivyo na siyo kujiingiza katika siasa pia.
Dk Bisimba alisema pia katika rasimu hiyo aliyoiita mpya, Bunge hilo Maalum la Katiba limeondoa maeneo yote yanayowagusa kwa namna moja ama nyingine huku akitolea mfano eneo la uwajibikaji.
Alisema katika eneo hilo katika rasimu za kwanza zilibainisha kuwa wabunge kwa kuwa wabunge wengi hawafanyi vizuri katika kipindi chao cha miaka mitano cha kuwatumia wananchi kutokana na kutoguswa kisheria, Katiba mpya itamke wazi kuwa mbunge atakayeshindwa kuwatumikia wananchi aondolewe achaguliwe mwingine.
Alisema katika rasimu hiyo mpya kipengele hicho kimeondolewa na kwamba mbunge bado anaendelea kuwatumia wananchi kwa kipindi chote bila kufanywa lolote hata kama hawajibiki.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ayoub Rioba, alisema Bunge hilo la Katiba ni kama vile limetunga rasimu mpya kwa kuwa limezifanyia mapinduzi rasimu zote zilizopita.
“Mchakato wote una tatizo, ulianza na kuundwa kwa tume ya Rais kukusanya maoni, maoni hayo yakatengenezewa rasimu, ambayo ikapelekwa bungeni ambako Bunge lingeirudisha kwa wananchi, lakini ikiwa bungeni imefanyiwa mapinduzi kwa kweli sina la zaidi,” alisema Rioba.
Mambo ya Muungano Kuhusu mambo ya Muungano, Mkurugenzi wa Utetezi maboresho na Sheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kuongezeka kwa masuala hayo kunatokana na kubomoa uliokuwa muundo wa serikali tatu na kuwa mbili.
Anasema misingi ya mambo ya katiba yanatokana na muundo, uliokuwepo tangu mwaka 1964 na kwamba jambo la muhimu wangeyavunja hayo kwanza kabla ya kuongeza hayo yaliyoongezeka.
Alisema suala zima la Muungano, lingerudishwa kwa wananchi na kupigiwa kura kwanza kabla ya kuhitimishwa katika rasimu hiyo.
Mambo hayo ya Muungano yaliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ni pamoja na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na usalama, usalama na usafiri wa anga, urais na uhamiaji, jeshi la polisi, sarafu na benki kuu, kodi ya mapato inayolipwa a watu binafsi na mashirika na ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zilizotengenezwa nchini na kusimamiwa na idara ya forodha.
Mambo mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, mahakama ya juu na mahakama ya rufani, elimu ya juu, baraza la taifa la mitihani na mambo yote yanayohusika na baraza hilo, utabiri wa hali ya hewa na utumishi katika serikali ya jamhuri ya Muungano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya hali ya Hewa nchini (TMA) Dk Agnes Kijazi alipongeza kuongezeka kwa mambo ya Muungano, kwani kutatoa mwanya mpana wa kufanya kazi za hali ya hewa. Alisema suala la hali ya hewa halina mipaka, ambapo kuwa mojawapo katika Muungano litasaidia katika uwekaji wa vifaa na kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wote.
Aidha, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya alipongeza rasimu hiyo kuzingatia kwa kwa kiwango kikubwa suala la usawa wa jinsia.
Alisema yapo mengi yaliyozingatiwa yanayohusu usawa wa jinsia likiwemo la uwakilishi katika uongozi, haki mbalimbali katika kumiliki na kutumia ardhi, afya ya uzazi salama, umri wa mtoto wa kike kufafanuliwa, kutambua lugha mbadala za alama kwa ajili ya watu wenye ulemavu pia na haki za makundi mbalimbali.
Imeandikwa na Halima Mlacha, Theopista Nsanzugwanko, Ikunda Erick na Lucy Lyatuu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!