Morogoro. Polisi mkoani hapa imefanikiwa kumkamata raia wa Burundi akiwa na baruti 10, darubini, hema, visu 10 na minyororo ya misumari kwa ajili ya kutega barabarani kufanikisha utekaji magari.
Akizungumza na waandishi jana, kamanda wa polisi mkoani hapa, Leonard Paulo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 31, mwaka huu saa 10:30 jioni akiwa Mtaa wa Makaburini B’, Mjimpya katika Manispaa ya Morogoro.
Kamanda Paulo alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na jitihada za polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Alisema baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu, ukiwamo ujambazi, utekaji wa magari na ulipuaji wa maeneo tofauti nchini.
Hata hivyo, alidai kuwa aliamua kujihusisha na uhalifu huo kutokana na ugumu wa maisha, hivyo ujambazi huo ulimsaidia kupata fedha.
No comments:
Post a Comment