Thursday 18 September 2014

AJALI YA MUSOMA: "NILISHUHUDIA WATU WAKITUPWA HUKU NA KULE"

“Kama ambaye nilikuwa nikitazama filamu ya kutisha, nilishuhudi watu wakirushwa huku na huko, vilio na kelele za kukata tamaa zikisikika kila kona, sikujua kitu gani kilikuwa kinatokea mpaka baada ya muda fulani kupita,”
 anasimulia Asha Juma (19), mkazi wa Nyakato, Musoma aliyekuwa abiria kwenye basi la Mwanza Coach lililogongana na J4 Express hivi karibuni.
“Majeraha makubwa na damu iliyokuwa ikichuruzika kutoka katika miili ya watu ilifanya nifikiche macho yangu kila mara ili kujiaminisha kile ninachokiona mbele yangu.”
Anasema hakutegemea safari yake ya kwenda Mwanza ingefupishwa ghafla namna ile.
Katika ajali hiyo iliyotokea Septemba mwaka huu, zaidi ya watu 37 walifariki dunia na wengine 78 kujeruhiwa vibaya. Ajali hiyo ilihusisha mabasi ya Mwanza Coach na J4 Express.
Asha anaeleza kuwa anakumbuka siku ya tukio alikuwa amepanda Mwanza Coach lililokuwa likielekea mkoani Mwanza. Alikuwa akienda kwenye shughuli zake. Anasema baada ya basi kwenda kwa muda wa nusu saa tu, lilitokea tukio la kutisha ambalo linamfanya aendelee kuhisi labda yupo ndotoni.
Anasema anakumbuka alikuwa kwenye kiti cha pili kutoka mwisho, kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kuona kilichokuwa kikitokea mbele yao na badala yake alishtukia kishindo kikubwa na baadaye viti vya mbele kung’ooka na kuwaponda waliokuwa wamekaa nyuma.
Asha anasimulia kuwa alishuhudia watu wakiwa na majeraha ya ajabu wakiwa wametapaa damu kila mahali huku wengi wao wakilia kwa uchungu na wengine wakionekana kukata roho.
“Kwa kweli ajali ilikuwa ni mbaya,” anasema. “Nilimshuhudia baba mmoja akiwa amekatika shingo na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili… niliogopa sana na kushikwa na butwaa, nikawa kama vile sielewi kinachoendelea.”
Anasema kuwa baadaye aliungana na abiria wengine waliokuwa wakilia kuomba msaada baada ya yeye na wengine watatu kuokolewa na watu wasiowafahamu kwa kupitishwa madirisha ya nyuma.
Binti huyo anasema hajui alinusurika vipi katika ajali hiyo kwani abiria wenzake wengi aliokaa nao viti vya nyuma nao walipoteza maisha.
Naye majeruhi mwingine, Frank Samson (35) mkazi wa Mwanza ni miongoni mwa walionusurika katika ajali hiyo mbaya ambaye anaeleza namna alivyoshuhudia ajali hiyo.
Frank, ambaye siku ya tukio alikuwa akisafiri na basi la Mwanza Coach akitokea Musoma kwenda Mwanza, anasema kuwa siku hiyo walianza safari saa 4:30 asubuhi wakitokea kituo kikuu cha mabasi iliyopo eneo la Bweri mjini Musoma.
Anasema kuwa dakika chache baada ya kufika Kitongoji cha Irimba Kijiji cha Sabasaba, ghafla gari dogo aina ya Land Cruiser lenye rangi nyeusi lilipita basi lao, likiwa katika mwendokasi bila kuchukua tahadhari ya aina yoyote.
Anasema kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani, gari hilo dogo lilipaswa kusubiri kwanza kabla ya kuchukua uamuzi wa kulipita basi kwa vile eneo hilo ni lenye mteremko mkali na kuna daraja, lakini dereva wa gari hilo hakuzingatia hilo.
Anaeleza kuwa wakati gari hilo likiwa katika harakati za kulivuka basi lao, ghafla walikutana na basi jingine la J4 lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Sirari wilayani Tarime.
Kama ilivyokuwa kwa upande wao, kufumba na kufumbua gari dogo liligongwa na mabasi yote mawili kwa ubavuni na kurushwa mtoni.
Anasema baada ya gari hilo kugongwa, mabasi hayo mawili yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vingi na majeruhi wengi. Anasema ajali hiyo ilitokana na mwendo wa mabasi hayo hasa ikizingatiwa kuwa yote yalikuwa kwenye mteremko mkali.
Frank anafafanua kuwa, baada ya ajali hiyo hakumbuki kilichoendelea kwani alipoteza fahamu na kujikuta akiwa amezungukwa na watu huku akiwa amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Akiongea kwa uchungu, anasema kuwa katika ajali hiyo wafanyakazi wenzake wote wa basi hilo, ambao ni dereva na utingo, walipoteza maisha papo hapo.
“Inaniuma sana wafanyakazi wenzangu tuliokuwa nao katika basi kupoteza maisha. Sijui ilikuwaje nikanusurika, kikubwa namshukuru sana Mungu,” anafafanua kwa huzuni.
Anasema kuwa kupona kwake ni muujiza wa Mungu kwani tukio hilo lilikuwa kubwa hasa ukizingatia idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kuongeza kuwa hana cha kumlipa Mungu zaidi ya kusema ahsante.
Ajali ya kihistoria
Ajali hiyo inasemekana imevunja rekodi ya ajali zilizowahi kutokea mkoani Mara kwa kipindi cha zaidi ya miaka 19.
Ajali kubwa kuwahi kutokea ilihusisha basi la Busigasore lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Musoma. Basi hilo lilipoteza mwelekeo wakati likijaribu kukwepa gari dogo aina ya Land Rover 109 katika eneo la Kiabakari wilayani Butiama mwaka 1995.
Katika ajali hiyo jumla ya watu 35 walipoteza maisha huku idadi kubwa ya watu wakijeruhiwa.
Vifo vya ajali
Jumla ya watu 1,126 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani katika kipindi cha miezi mitatu huku kukiwa na majeruhi 3,827 kati ya ajali 3338 zilizotokea katika maeneo tofauti nchini.
Takwimu hizo zilitolewa wiki iliyopita na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe alipokuwa akifungua mkutano wa mazungumzo ya pamoja na wamiliki wa mabasi ya kusafirisha abiria.
Dk Mwakyembe alisema katika ajali hizo, zaidi ya asilimia 90 zilitokana na uzembe wa madereva ambao wengi wamekuwa hawajali sheria za barabarani ikiwamo kuendesha vyombo hivyo wakiwa wamelewa.
Waziri alitaja ajali hizo kwamba zilitokea katika kipindi cha Juni Mosi hadi Septemba 8 na kwamba kila mwezi kulikuwa na ongezeko la vifo.
“Juni tulipata ajali 1,157, zikasababisha vifo vya watu 320 na majeruhi 1,189, Julai zilikuwa ajali 1,035, vifo vikawa 368 na majeruhi 1,261 wakati Agosti ajali zilikuwa 1,146 kukawa na vifo 390 na majeruhi 1,365,” alisema Mwakyembe.
Waziri alisema kipindi hiki siyo cha kulaumiana na badala yake kila mmoja atimize wajibu kwa kuwa Watanzania wanaangamia.
Kiongozi huyo aliwataka wamiliki kutulia na kufanya uchambuzi wa kina juu ya nini kinasababisha ajali kuongezeka mwezi hadi mwezi na kuwa karibu na madereva na watumishi wengine kwenye mabasi.
Akizungumza katika Mkutano huo, Katibu wa Chama cha Wenye Mabasi (Taboa) Enea Mrutu alikiri ajali nyingi kusababishwa na uzembe wa madereva ingawa yeye alisema ni kwa asilimia 70.
Hata hivyo, Mrutu alisema bado kuna kazi katika vyombo vya usimamizi ikiwamo polisi ambao wamekuwa wakiwanyanyasa madereva na kuwachelewesha jambo linalofanya kuongeza mwendo wanapoachiwa.
Kingine Katibu huyo alilalamikia ni vyuo vya usafiri ambavyo hutoa madereva ambao mwishowe wanaonekana kutokukidhi viwango wakati vyuo hivyo vipo chini ya Serikali.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!