DESEMBA mwaka 2002, nilitoa mada juu ya Ukimwi, katika Kongomano la kimataifa juu ya Ukimwi, lililofanyikia Arusha. Kwa unyenyekevu mkubwa niliunga mkono matumizi ya kondomu, kama njia mojawapo ya kuzuia kuenea kwa Ukimwi.
Sambamba na maoni yangu niliungana na Padre Joinet, kwa pendekezo lake la Mashua tatu: Uaminifu, kujinyima au kutumia kondomu. Haikuwa rahisi kwa padre Mkatoliki, kukubaliana na matumizi ya kondomu na kutamka hadharani juu ya jambo hili. Nilishutumiwa na kulaaniwa na watu wengi na niliadabishwa kwa nguvu zote na viongozi wa Kanisa Katoliki.
Hadi leo hii sijagundua kosa nililolifanya. Ninasali, ninatafakari na kumuomba Mwenyezi Mungu, kunijalia ujasiri wa kupiga magoti na kuomba toba mbele ya viongozi wangu, waheshimiwa maaskofu wa kanisa katoliki la Tanzania.
Mungu, amekaa kimya! Ukimwi, unaendelea kusambaa kwa kasi.Watoto yatima, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanaongezeka kila kukicha.
Watoto wanabakwa, wanarubuniwa kwa pesa kufanya mapenzi katika umri mdogo, nyumba ndogo zinaibuka na kuzagaa, ngono linakuwa jambo la kawaida kama starehe nyingine zote.
Baadhi ya watu walionilaani kwa kitendo changu cha kuunga mkono matumizi ya kondomu wamekufa au wameambukizwa Ukimwi, na wengine wamekumbwa na kashifa za ngono, kuwadhalilisha watoto na kufanya ngono kinyume na maumbile!
Mwaka 2004, Benki ya dunia iliendasha utafiti juu ya Ukimwi na Uchumi Mkoa wa Kagera, nilipata bahati ya kushiriki utatifi huu uliochukua muda wa mwaka mzima.
Utafiti huu ulinipatia mwanga mkubwa juu ya ugonjwa wa Ukimwi na kunipatia nguvu za kujiamini zaidi juu ya msimamo wangu wa kuunga mkono matumizi ya kondomu kama njia mojawapo ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi.
Katika utafiti huo, nilishangaa sana kugundua kwamba idadi kubwa ya watu wa mkoa wa Kagera, hawakukubali kwamba ugonjwa wa Ukimwi, lilikuwa ni janga. Bila kutambua kwamba ugonjwa huu ni janga, inawezekana watu kuwa wangalifu katika kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huu?
Watu wanaamini ngono bila mpangilio ni dhambi lakini kutumia kondomu ni dhambi mara mbili! Dini inazuia utumiaji wa kondomu, jambo hili linawaingia vichwani watu wa vijijini.
Kule vijijini watu wanawaamini sana viongozi wa dini, hivyo wanaamua kutenda dhambi ndogo ya kutenda tendo la ngono bila kutumia kondomu.
Matokeo yake ni wajane na watoto yatima! Nilishangaa pia kugundua kwamba vijijini watu wanaishi kwenye umasikini usikokuwa wa kawaida. Mche wa sabuni au kilo moja ya sukari inatosha kumlazimisha mtoto yatima wa kike kufanya ngono.
Binti mmoja alituelezea jinsi alivyolazimika kufanya tendo la ngono bila kinga ili apate pesa za kulipia matibabu ya wadogo zake aliokuwa akiwatunza. Afya yake haikuwa nzuri, na bado alikuwa na jukumu la kumlea mtoto wake mdogo na wadogo zake watano.
Mwaka huu mwezi wa nane, nimepata bahati ya kufanya tena utafiti juu ya watoto yatima, wajane na urithi wa ardhi na mali za marehemu, katika wilaya ya Muleba, mkoa wa Kagera.
Utafiti huu umenipatia nafasi ya kuvizungukia baadhi ya vijiji ambavyo sikuvizungukia wakati wa utafiti wa 2004. Vijiji hivi ni vile vilivyo kando kando mwa Ziwa Victoria.
Vijiji hivi ni vile ambavyo wakaaji wake wengi ni wavuvi. Hawa wameguswa na utandawazi wa kila aina. Samaki wao wa miaka mingi wamekwenda na utandawazi. Utandawazi umeleta wageni kwenye vijiji na visiwa vya Muleba na kusababisha kasi ya kusambaa kwa virusi vya Ukimwi.
Ukimwi unaendelea kusambaa, watoto yatima wanaongezeka, ujinga na umasikini vinaendelea kuwa kitanzi cha jamii. Yatima wanaendelea kuwalea yatima na mbaya zaidi ni kwamba sasa yatima wanazalisha yatima.
Yatima, wanazalisha yatima! Labda hili ndilo jipya. Ingawa yatima na watoto walio katika mazingira magumu wana matatizo mengi, tatizo la yatima kuzalisha yatima ni changamoto katika taifa letu.
Tumezoea matatizo ya watoto yatima kudhurumiwa mali zao, kunyimwa haki ya kwenda shule, kubakwa, kufanyishwa kazi ngumu, kutumiwa kama mradi wa mapato kwa walezi wao.
Kwa vile yatima walio wengi hawapati bahati ya kwenda shule, baadhi wanaishia dara la saba na wengine hawaendi shule kabisa, wanaoa na kuolewa katika umri mdogo.
Kule Muleba, nimeshuhudia baadhi ya watoto yatima wenye umri wa miaka 22, wamekwisha poteza waume zao na wanalea yatima.Wao ni yatima, na sasa wanazalisha na kulea yatima. Bila mikakati na mifumo ya maadili iliyo wazi na mizuri, huu utakuwa ni mnyororo usiokatika.
Tutaendelea kuwa na kizazi cha yatima kinachozalisha yatima na kuwa na jamii ya watu wasiozidi umri wa miaka 25 hadi 30.
Kwanini yatima wanazalisha yatima? Yapo majibu mengi. Ulinzi na uangalizi wa watoto yatima ni mdogo. Jamii, serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali imeshindwa kuunda mifumo mizuri ya kuangalia usalama na makuzi ya watoto yatima.
Kinachozingatiwa ni misaada zaidi ya ulinzi na makuzi. Lakini kubwa ya yote ni kwamba Ujinga na umasikini ni vyanzo vya ndoa za mapema kwa watoto yatima.
Kati ya watoto yatima kumi wilaya ya Muleba nilioongea nao, ni mmoja tu aliyemaliza kidato cha nne naye alikuwa mjane (24) akiwa na watoto watatu! Wengi wao wamemaliza darasa la saba na wengine hawakwenda shule kabisa.
Baada ya darasa la saba na wengine wanapofikisha umri wa miaka 12, watoto wanakimbilia visiwani kutafuta kazi. Wasichana wanaishia kuuza miili yao ili wapate pesa za kuwatunza wao na wadogo zao. Matokeo yake wanabebeshwa mimba na wengine wanaolewa na watu walioathirika. Wanapopata watoto wawili au watatu, waume zao wanakufa! Hawa wasichana waliokimbilia visiwani wanarudi vijijini kuendelea kulea yatima katika mazingira magumu.
Ili kupata matumizi wanalazimika kutembea na kila anayeweza kutoa matumizi bila kuzingatia kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi. Hawapendi kupima, ili kujua hali ya afya zao, la msingi kwao ni kupata pesa za kuwatunza watoto wao.
Mbali na tatizo kubwa la yatima kuzalisha yatima, kuna tatizo jingine linalojitokeza kwa nguvu.Tatizo hili ni ngono kuwa kitu cha kawaida, kitu ambacho sasa hivi kinafanyika bila maadili yoyote yale.
Ni kweli kwamba ngono ni hitaji la kila binadamu aliyetimamu. Iwe kwa uwazi, kujificha au kwa unafiki, ngono ni hitaji la kila binadamu. Ni tendo la heshima ambalo ni lazima lifanyike kwa maadili mazuri.
Sasa hivi ni kinyume watu wazima wanafanya mapenzi na watoto wadogo na hasa watoto yatima ambao hawana ulinzi na uangalizi wa kutosha. Tendo ambalo ni lazima kufanyika kwa upendo na uwajibikaji wa hali ya juu, linafanyika ovyo ovyo na wakati mwingine kwa nia mbaya.
Tofauti na siku za nyuma, sasa hivi hata watoto wa shule za msingi wamekwishadumbukia katika matendo ya ngono. Wito kwamba watoto hawa wafundishwe elimu juu ya miili yao na jinsi ya kujikinga na Ukimwi, si wa kupuuzwa.
Wataalamu wanakubaliana kwamba kwa kiasi kikubwa Ukimwi unaenea kupitia katika tendo la ngono. Hivyo mtu anayetaka kupambana na Ukimwi ni lazima ashughulike kwa nguvu zote kutengeneza mifumo ya kuongoza maadili ya ngono na kuongoza uhusiano wa mtu na mtu.
Bila kuwa na maadili mazuri ya mahusiano, bila majadiliano ya wazi juu ya ngono, bila elimu ya kutosha juu ya mapenzi, ngono na uwajibikaji, kupambana na Ukimwi, ni ndoto.
Tutaendelea kuzalisha watoto yatima na watoto yatima kuzalisha yatima. Tutaendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa, na uchumi wa taifa letu utaendelea kudidimia.
Hivyo changamoto ya jamii yetu, serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, ni kutengeneza mfumo wa kuongoza maadili ya ngono. Mbali na hili la maadili ni kukazania elimu.
Ni kuhakikisha vijana na hasa watoto yatima wanapata elimu ya kutosha. Miaka mingi katika shule inaweza kuepusha balaa la watoto yatima kuolewa katika umri mdogo.
Lakini changamoto kubwa kuliko zote ni umasikini. Kupambana na Ukimwi, kuwatetea na kulinda usalama wa watoto yatima na watoto walio katika mazingira magumu ni kupambana na umasikini.
Hali ya uchumi ingekuwa nzuri wasichana wanaolazimishwa kufanya ngono zembe ili wapate pesa nyingi zaidi, wasingefanya hivyo. Hali ya uchumi ingekuwa nzuri watoto wasingefanyishwa kazi ngumu. Hali mbaya ya uchumi inasababisha maovu mengi katika jamii yetu.
Hatuwezi kupambana na umasikini kwa kuendesha semina za Ukimwi, na kumwaga mapesa mengi ambayo mara nyingi hayadondoki mikononi mwa yatima,wajane na waathirika wa Ukimwi.
Hatuwezi kupambana na umasikini kwa kutoa misaada kwa watoto yatima, ambayo kwa kiasi kikubwa inayeyuka mikononi mwa walezi wa watoto yatima.
Hatuwezi kupambana na umasikini kwa kugawa ARV, ambazo baadhi ya waathirika wanaziuza kupata pesa za kununua chakula. Tunaweza kupambana na umaskini kwa kubuni sera nzuri za kukuza uchumi wetu kwa kujali uhai wa kila Mtanzania!
Kama taifa letu linalenga kupunguza ongezeko la watoto yatima na kupambana na Ukimwi, ni lazima taifa letu lipambane kikamilifu na ujinga, umaskini na kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi. Haya ni mapambano ya muda mrefu na mapambano yanayodai juhudi za kila mtanzania.
La haraka zaidi ni kuzuia kuenea kwa virusi. Hili linaweza kufanyika kwa njia mbali mbali – njia zote ni ngumu na zinahitaji uamuzi, mifumo, maadali na kusaidiana. Zaidi ya yote njia zote zinahitaji uwazi na uwajibikaji. Uaminifu, ni njia ambayo ni ngumu, Mungu, alificha undani wa mtu, hivyo mtu binafsi bila msaada wa ndugu, marafiki na viongozi wa kiroho, hawezi kutunza auaminifu kwa mwenzake.
Uaminifu anaendana na kuvumiliana na kuchukuliana, haya yanawezekana kwa msaada wa wengine. Watu wengi wanajigamba kuwa waaminifu, na kutembea njia yao wenyewe, lakini matokeo yake ni mauti na kuzalisha watoto yatima!
Kujinyima nako ni kitu kigumu kwa mtu anayeishi na watu, labda mtu anayeishi peke yake akizungukwa na vitu visivyokuwa na uhai, tuna mifano mingi ya watu wanaoshi maisha ya kujinyima, lakini wanaambukizwa virusi!
Kutumia kondomu, nako ni kugumu, bila ushauri na elimu ya kutosha. Wengine wanaanza kwa kutumia kondomu, wakizoeana wanaacha. Virusi, havipotei kwasababu ya kuzoeana! Au wengine wanazitumia kondomu vibaya. Hata hivyo kama kuna elimu ya kutosha na uwazi unaozingatia umuhimu wa wa uhai, matumizi ya kondomu yanaweza kuzuia kasi ya kuenea kwa virusi zaidi ya uaminifu na kujinyima vitu ambavyo mara nyingi vinazungukwa na unafiki wenye nguvu zaidi ya kifo!
VIA-TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment