Rais Jakaya Kikwete amewakosoa Watanzania wanaoishi ughaibuni kwa kile alichoeleza kuwa wameshindwa kujenga hoja ya kuwashawishi Watanzania wenzao kuhusu umuhimu wa kuwa na uraia pacha katika Katiba Mpya.
Rais Kikwete anayasema hayo wakati akihutubia mkutano wa kwanza wa kihistoria na diaspora uliofanyika Agosti 14 na 15. Mkutano huo uliwakutanisha Watanzania wanaoishi katika nchi 17 duniani, ulioandaliwa na Asasi ya Tanzania Diaspora Initiative (TDI), chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji, Emmanuel Mwachullah.
Suala hili la uraia pacha, limejitokeza na kuwa changamoto, ambapo Watanzania wanaoishi ughaibuni, wameelezea jinsi wanavyokosa fursa za kushiriki katika maendeleo mbalimbali ya nchi.
Watanzania hao wanasema kuwa wanashindwa kuwekeza, kurudi au hata kusaidia familia zao kwa sababu mbalimbali, ikiwamo za usumbufu na kupanda kwa gharama za maisha.
Katika mazungumzo hayo Rais Kikwete anasema kukosekana kwa ushawishi juu ya suala hilo kumefanya lishindwe kupewa kipaumbele katika mjadala wa katiba unaoendelea kwa kuwa haliwakeri wananchi wengi.
“Jambo ambalo pia ni muhimu kulifanya ni kuwashawishi wajumbe wa Bunge la Katiba ili wakubali hoja zenu za uraia pacha kuwa ndani ya katiba, hili siyo jambo haramu. Zungumzeni nao Serikali haina tatizo iwapo Katiba itawatambua,” anasema Kikwete.
Rais Kikwete anawashauri Watanzania hao kutumia muda wao, kujenga hoja zao hata kwenye mitandao ya kijamii, badala ya kubishania mambo ya kisiasa zaidi.
“Suala la uraia lipo katika katiba, siyo jambo ambalo eti mimi kwa nafasi yangu kama rais ninaweza kutangaza, kwamba kuwepo na uraia pacha kisha iwe hivyo. Mnatakiwa kuendelea kulizungumza ili jamii ielewe faida zake na ione umuhimu wa kuwepo kwenye Katiba,” anasema Kikwete.
Rais anasisitiza kuwa Watanzania hao wasijipe matumaini kwa sababu kwa namna ilivyo, rasimu ya Katiba Mpya haiwezi kuzaa uraia pacha. Rasimu ya Katiba iliyopo inazungumzia hadhi ya Watanzania walioko nje ya nchi na siyo uraia,” anasema.
Rais Kikwete anasema tatizo linaloonekana wazi ni kwamba suala hilo halikujitokeza sana katika mijadala ya mabadiliko haya ya Katiba na kwamba si suala linalofurahisha.
Anasema suala hilo limewahi kujadiliwa hata ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kukafanyika juhudi za kujaribu kuliingiza kama hoja muhimu, lakini lilionekana kutokuwa na nguvu ya kutosha kwa kuwa hakukuwepo na wahusika wanaoguswa na suala hilo moja kwa moja.
“Nilimchagua kadiri Singo ambaye anawawakilisha kwenye Bunge la Katiba lakini yeye pekee yake hatoshi kufanya jambo hili lionekane umuhimu wake, nilifikiri kwamba mngetumia vyema mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe lakini kumekuwa kimya,” anasema Rais Kikwete
Alisema kwa hatua yoyote watakayochukua kwa ajili ya kutafuta na kuongeza ushawishi wa suala hilo katika jitihada za kutaka litambuliwe kikatiba itakua sahihi , kwa kuwa siyo jambo baya hata ikibidi kwenda kuwaona wabunge na kuwaeleza kwamba waliangalie kwa umuhimu wake.
“Sisi upande wa Serikali tunaliona ni suala jema, ila halina nguvu kwa sababu wabunge wengi haliwagusi moja kwa moja hivyo si rahisi kulipigania. Mbona nchi nyingine watu wao wananufaika na hili sasa kwa nini hapa kwetu lishindikane?” alihoji.
Hatua iliyofikiwa ndani ya Bunge la Katiba
Watanzania hao walioko nje ya nchi, Machi mwaka huu walituma waraka maalumu kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ikiwa ni jitihada mojawapo za kutilia mkazo suala hilo liingizwe kwenye katiba mpya.
Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad, alisema raia hao wameomba waraka huo ujadiliwe na wajumbe wakati huu ambapo mchakato wa kuandika Katiba unaendelea katika kamati.
“Raia walioko nje ya nchi, wametuma waraka maalumu ambao waliomba ujadiliwe ndani ya kamati kuhusiana na uraia pacha na walimtuma mjumbe anayewawakilisha Kadiri Singo .
Kutokana na umuhimu wa suala hilo, alisema alimuomba Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta, aruhusu waraka huo ujadiliwe ndani ya kamati na alipewa ruhusa ya kufanya hivyo.
Akizungumzia suala la uraia huo, Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Paul Kimiti, alisema wamejadili suala hilo kwa kina na kulipitisha.
Anasema ibara hiyo ilikuwa na mvutano, hasa kwa upande wa Zanzibar ambapo baadhi ya wajumbe wamekuwa na hisia tofauti kuhusu kuruhusu uraia pacha.
“Baadhi ya wajumbe wameonyesha hofu yao, hasa kwa watu waliotorokea nje ya nchi wakati wa mapinduzi na kwamba kuwaruhusu kuwa na uraia pacha kunaweza kuleta matatizo,” anasema.
Kimiti anasema wajumbe walipendekeza kuwapo uraia pacha kwa makubaliano ya kutungwa sheria ya kudhibiti utolewaji wake
Faida za uraia pacha
Kwa upande wake Singo anasema kuwa uraia pacha una faida kwao na nchi kwa jumla, kwa sababu ndiyo utakaotanua wigo wa kuwawezesha kushiriki vyema katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“Kwa kutokuwa na uraia wa nchi tunazoishi kuna fursa nyingi tunazikosa, ikilinganishwa na wenzetu wanaotoka katika nchi zinazoruhusu uraia wa aina hii, lakini sisi tunabanwa na kupoteza haki ya kupata huduma muhimu za kijamii katika maeneo tunayoishi,” anasema.
Anasema kuwa wamekuwa na jukumu la kuitangaza nchi katika maeneo wanayoishi, hivyo kuwezesha nchi kupata watalii, hivyo kuongeza pato la taifa.
“Tukiwa kule nje tunatangaza Kiswahili, utamaduni sisi ndiyo tunaowapokea viongozi wetu wanapotembelea nchi husika, tusiwe wavivu wa kufikiria kuhusu uraia pacha, idadi ya watu wanaokadiriwa wanaishi nje ya nchi ni milioni 3 hivyo ni wengi,” anasema Singo
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment