WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti jijini Dar es Salaam, likiwemo la mtoto Susan Shadrack (2) mkazi wa Majohe Kivule aliyetumbukia kisimani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni wakati mama yake, Maria Shadrack alipokwenda kuokota kuni.
Alisema kunwa mzazi huyo aliporudi, hakumkuta mtoto wake na baada ya jitihada za kumtafuta ndipo walipobaini ametumbukia katika kisima kilichopo nyumbani kwao.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kibamba, Mwajuma Hamis (42) amefariki dunia baada ya kuungua moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku baada ya moto kuzuka ghafla katika nyumba ya Clara Henry (24), yenye vyumba sita na kuteketeza vyumba vitatu na vitu vilivyokuwemo ndani.
Wambura aliongeza kuwa, katika tukio hilo marehemu aliungulia ndani ya nyumba hiyo hali iliyosababisha kifo chake.
Alisema kuwa chanzo na thamani za mali iliyoteketea bado haijafahamika, mwili umehifadhiwa katika hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani
No comments:
Post a Comment