WAGANGA wa Tiba Asili wamehamasishwa kujiepusha na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina na uchawi kama vyanzo vya ugonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema zipo taarifa na migongano mingi ya kutisha juu ya jambo hilo, hivyo ni busara kwa waganga wa tiba asilia kupitia kwenye vyama vyao, kupanga mikakati ya kudhibiti na kuondoa vitendo hivyo.
“Wizara inatambua kuwa ujuzi wa tiba asili ni taaluma rasmi, vitendo hivyo vibaya vinachafua taaluma hii, nawashauri waganga kubadilika na kwenda na wakati kwa kuwa sasa yapo mazingira mazuri yanayoshirikisha maendeleo ya tiba asili katika mabadiliko yanayoendelea kwenye sekta ya Afya,” alisema.
Alisema changamoto iliyopo nchini ni jinsi miti dawa inaweza kufanyiwa utafiti na kuwa dawa bora na salama kwa watumiaji, ambako kuna miti dawa mingi na kati ya hiyo haijafanyiwa utafiti na kuweza kubaini uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali.
Aidha, Waziri Seif alisema Agosti 31 kila mwaka, nchi 46 za Kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya duniani, huadhimisha siku ya tiba asilia ya Mwafrika, na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘ushirikiano kati ya watoa huduma wa tiba asili na tiba ya kisasa’.
Aidha, aliwataka waganga wa tiba asili kujiepusha na matangazo yanayokinzana na taarifa za kiutafiti katika suala zima la kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali, mfano Ukimwi.
No comments:
Post a Comment