Historia ya vita ya Majimaji imekuwa ikielezwa kwa namna mbalimbali. Kila mmoja anasimulia kwa namna alivyosikia. Wananchi wengi wa ukanda wa kusini walikimbia vita na kuishi sehemu tofauti tofauti na kila mtu amekuwa akisimulia anavyojua ama alivyosimuliwa.
Nikapata shauku ya kufuatilia historia hiyo katika mji maarufu wa Ngarambe, inavyoelezwa kuwa huko ndiko alikozaliwa Kinjeketile Ngwale pia ni huko ambako alianzisha harakati zake za kukabiliana na mkoloni Mjerumani.
Nalazimika kuanza safari kutoka jijini Dar es Salaam hadi wilayani Rufiji katika Mji wa Utete yalipo Makao Makuu ya wilaya umbali wa kilometa 201 na nilipouliza nikaelekezwa kilipo Kijiji cha Ngarambe. Wenyeji katika mji wa Utete walinieleza kwamba nalitakiwa nisafiri tena kuelekea Ngarambe umbali wa Kilometa 65. Usafiri katika maeneo hayo ni wa gari ambalo safari huanza saa 7.00 mchana.
Siku ya pili baada ya kupumzika nilianza safari kuelekea Ngarambe ambako nilipokewa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngarambe, Saidi Logolo ambaye katika mazungumzo yangu naye anasema kitongoji hiki awali kilikuwa kijiji na baada ya kuingizwa katika mamlaka ya mji mdogo wa Utete kimebadilika na kuwa kitongoji.
Nikamuuliza kama anajua chochote kuhusu historia ya mtu anayeitwa Kinjeketile Ngwale akanijibu kuwa anajua lakini akanishauri nisafiri tena umbali wa kilometa 15 katika Kijiji cha Ngarambi ambako ningepata historia nzuri ya kiongozi huyo wa vita ya Maji Maji kutoka katika ukoo wa Kinjeketile Ngwale uliopo katika Kijiji cha Ngarambi Wilaya ya Kilwa.
Mwenyekiti huyo anasema kuwa Ngarambe ipo upande wa Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani na Ngarambi ipo Wilaya ya Kilwa ni vijiji vilivyo mpakani vyenye majina yanayotofautiana herufi moja ya mwisho. Kwa wenyeji huviita Ngarambe Matingi na Ngarambi Lienga.
Kutoka Utete njiani kuna msitu mkubwa sana ambao umepewa jina la Kichi. Kichi ni kabila dogo sana katika ukanda huu ambalo limemezwa na Kabila la Wamatumbi hupenda kuishi katika misitu na chakula chao kikuu ni nyama.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kungurwe, Kata ya Ngarambe, Ali Matimbwa anasema kuwa msitu huo awali walikuwa wakiishi kabila dogo sana la Kichi na ndio maana ukapewa jina la Kichi.
Matimbwa anasema kuwa kabila hilo linafanana sana na Wahadzabe na Wasandawe kutokana na kupenda kwao kula nyama za porini lakini sasa kabila hilo limemezwa na makabila ya Wangindo na Wamatumbi.
Safari ya kwenda Ngarambi ilianza kwa kutumia usafiri wa pikipiki nilipoingia katika kijiji hicho kilichopo juu ya mlima kikiwa na nyumba chache za bati na nyingi za nyasi na zilizojengwa kwa tope. Nilijitambulisha kwa wenyeji wangu ambao ni Mwenyekiti wa Kijiji, Hemedi Kapunju.
Nilitaka kujua kama anafahamu lolote kuhusu Kinjeketile Ngwale alijibu kuwa alizaliwa katika Kijiji cha Ngarambi katika Kitongoji cha Kinjeketile kilichopo Kata ya Kandawale, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Kapunju anaanza kwa kunihoji kama nina mazungumzo marefu kwani ana kazi ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupata vitambulisho vya uraia. Hata hivyo, anamuaga ofisa mtendaji wa kijiji kwamba atakuwa na mazungumzo nami kwa muda, wakakubaliana na mtendaji wake.
Anasema kuwa Kijiji cha Ngarambi kina vitongoji viwili kimoja kinaitwa Kinjeketile kilichopo upande wa Mashariki na Magharibi kuna Kitongoji cha Nantote. Namuuliza mwenyekiti kwa nini kitongoji hiki kikaitwa Kinjeketile akanijibu kuwa kitongoji hiki kimepewa jina hilo kwa heshima ya mpiganaji huyo Kinjekitile Ngwale aliyezaliwa hapo.
Kapunju anaanza kwa kuelezea jiografia ya Kijiji cha Ngarambi na alisema kuwa kwa upande wa Mashariki kimepakana na Kijiji cha Kikobo, Kaskazini kimepakana na Kijiji cha Namakono, Magharibi kimepakana na Ngarambe vijiji ambavyo vipo Wilaya ya Rufiji na Kusini kimepakana na Kijiji cha Kandawale. Kina wakazi 457 tu na shughuli zao kuu ni kilimo cha ufuta, mahindi, mtama na mazao mengine jamii ya kunde.
Bi Halima Ngunja (80) mmoja wa wazee niliofanya mazungumzo nami anasema kuwa shujaa huyo alizaliwa hapa na ndio maana hata ukoo wa Ngwale bado upo hadi leo na baada ya kumalizika vita Kinjeketile alihamia Kibata na simulizi za wazee zinaeleza kuwa alifia huko.
Kinjeketile mganga maarufu, tishio
Bi Halima anasema kuwa masimulizi aliyoyapata kwa mzazi wake Nganoga ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Ngarambi anasema kuwa Kinjeketile alikuwa mganga maarufu sana na alikuwa tishio katika eneo hili.
“Alikuwa tishio sana mtaani hapa watu wengi walimuheshimu sana na watu mpaka leo wanakwenda kutambika katika eneo alikozaliwa,” alisema.
Hemedi Kapunju anasema kuwa simulizi za wazee walioshiriki vita na wale waliokimbia, wakati wa vita alikuwa akichukua maji yaliyokuwa yakitiririka katika jiwe katika milima iliyopo maeneo ya Kaumbwaga na kuyatia kwenye kibuyu fulani ambacho ndani ya kibuyu kuna dawa na kuwapa askari wake pindi wakivamiwa na maadui watumie kama kinga.
Wakati Kapunju akisema hayo anasema kuwa Kinjeketile alikuwa akitaka dawa anaingia ndani ya maji katika bwawa lililokuwa likiunganisha mito mitatu na alikuwa akikaa siku tatu huko na kutoka na dawa ambazo zilitumika kuwasadia askari wakati wa vita.
Anasema kuwa mara baada ya Wamatumbi kung’oa pamba ya Mjerumani huko Nandete askari wa Kijerumani waliwatandika vilivyo ndipo Wamatumbi wakaamua kukimbilia kwa Kinjeketile Ngwale kuomba msaada kwa kuwa alikuwa akiaminika kuwa ni mganga maarufu na mchawi wa hali ya juu ili kukabiliana na Mjerumani.
Vita baina ya Wamatumbi na Wajerumani
Kapunju anasema kuwa mwanzo wa Vita ya Majimaji huko Umatumbini ilikuwa ni mwendelezo wa vita ya muda mrefu kati ya utawala wa Wajerumani na Wamatumbi ambao walikuwa wamechoka kabisa kutawaliwa.
Anasema kuwa hiyo ilitokana na Wajerumani walioingia kama marafiki, kugeuka kuwa wakatili. Wamatumbi walichukizwa na kitendo cha kufanyishwa kazi katika mashamba ya pamba ya Wajerumani kutwa nzima bila malipo
Anasema kuwa hali hiyo ilijenga chuki kati ya Wamatumbi na Wajerumani, hivyo Wamatumbi walianzisha vita iliyokuwa ya Mzungu na Mmatumbi popote pale walipokuwa wakikutana.
Kapunju anasema kwa kuwa wajerumani waliongeza ukatili na wakaamuru Wamatumbi wote kuepukana na asili yao ya kutembea na fimbo, Serikali ya Mjerumani ilitunga sheria kwamba Mmatumbi yeyote anayepatikana akitembea na aina yoyote ya mti atakiona cha moto.
MWANANCHI.
1 comment:
aziz bilalYesterday 21:41
1
Reply
Lo,jamaa anafikiria ndio kaandika historia ya vita ya maji maji ,nimepitia hadithi yake fupi na nimegundua kuna mengi kashindwa
Post a Comment