Friday 22 August 2014

MAMA WA ALIYENG'ATWA NA MENO NA MWAJIRI ATOA USHAHIDI

Mama mzazi wa Yusta Lukas ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ya kujeruhi kwa meno inayomkabili Amina Maige, mkazi wa Mwananyamala kwa Manjunju jana aliieleza mahakama jinsi taarifa za kujeruhiwa kwa binti yake zilivyomfikia akiwa mkoani Tabora.
Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tumaini Mfikwa shahidi huyo, Modesta Simon, mbele ya Hakimu Yohana Yongolo alisema kuwa alizipata taarifa hizo kutoka kwa mwalimu wa shule ya sekondari iliyo jirani na nyumbani kwake baada ya habari za Yusta kudaiwa kuteswa na mwajiri wake kuenea katika vyombo mbalimbali vya habari.
Aliiambia mahakama baada ya taarifa hizo pamoja na kupokea simu kutoka polisi kwamba binti yake amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala alikata shauri ya kuja Dar es Salaam kwa kukopa nauli pamoja na michango ya ndugu zake.
Alisema baada ya kufika Dar es Salaam na kwenda hospitalini hapo alikolazwa mwanaye, alishtushwa na hali aliyomkuta nayo kwa kuwa alikuwa amedhohofu, mweusi kwa makovu na hawezi kuongea vizuri.
Aliendelea kuwa hali ile ilimchanganya sana na baada ya kumhoji nini kilichomtokea, alimwambia amekuwa akipigwa kwa muda mrefu na mwajiri wake Amina na amekuwa akikaa kimya bila kuripoti kutokana na hofu kwani alimtisha kumfanyia kitu kibaya endapo atasema.
Hata hivyo upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Emannuel Agustino ulidai mahakamani hapo kuwa shahidi huyo amekubali kufika mahakamani na kutoa ushahidi wake kwa kuwa ameahidiwa kiasi cha Sh20 milioni na kikundi cha kikoba kinachomhifadhi yeye na Yusta kwa sasa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 16 upande wa Jamhuri utaleta mashahidi wengine.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!