Friday 22 August 2014

BOMU LAUA WATATU, DEREVA WA JAJI AUAWA KATIKA MLIPUKO HUO


Watu watatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi, kurusha bomu ndani ya basi dogo aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitoka Kilelema kwenda Kasulu, Kigoma.

Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilelema, Benedicto Mahuta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00 alfajiri kwenye Pori la Kasesema, lililopo kati ya kijiji hicho na Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Migongo, Wilaya ya Buhigwe.
Mahuta alisema wakati gari hilo likipita eneo hilo, mtu mmoja alionekana amesimama katikati ya barabara huku ameshika bunduki, hali iliyomlazimu dereva kuongeza kasi.
Alisema hatua 15 baada ya kumpita, walimuona mtu mwingine akiwa amesimama pembeni mwa barabara na baada ya kumpita, abiria waliokuwa wameketi nyuma ya basi hilo walishtukia kitu kizito kikitupwa ndani.
Mmoja wa abiria aliamua kukirusha nje lakini kililipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na mtoto mdogo.
Mmoja wa abiria walionusurika, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kilelema, Augustino Mkubhaka alisema baada ya mlipuko huo, gari lilipelekwa katika kambi ya JWTZ kwa ukaguzi.
Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Buhigwe, Samwel Utonga alisema inasadikiwa kuwa watu waliorusha bomu hilo ni majambazi wanaotokea nchi jirani.
Dereva wa jaji EACJ auawa
Dereva wa mmoja wa majaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Ibrahim Msagati amefariki dunia kwa kupigwa risasi iliyofyatuka kutoka kwenye bastola ya mlinzi wa jumuiya hiyo.
Tukio hilo lililoibua majonzi na simanzi miongoni mwa wafanyakazi wa EAC lilitokea jana saa saba mchana muda mfupi baada ya kikosi cha ulinzi cha Jumuiya kumtia mbaroni mtu mmoja aliyefika Makao Makuu ya EAC kwa tuhuma ambazo hazikujulikana mara moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema tukio hilo ni la bahati mbaya kwani risasi ilifyatuka kutoka kwenye silaha ya mmoja wa maofisa usalama wa EAC.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma wa EAC, Richard Otieno-Owora alimtaja ofisa usalama ambaye risasi ilifyatuka kutoka kwenye bastola yake kuwa ni Jackson Oula.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!