Sunday, 31 August 2014
JESHI LA JWTZ KULINDA ALBINO
JESHI la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kikosi cha 516 , cha kambi ya Kizumbi mkoani Shinyanga, limeahidi kuwahakikishia ulinzi na usalama watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaolelewa katika kituo cha Buhangija Jumuishi kilichopo Manispaa ya Shinyanga.
Hayo yalibainishwa kituoni hapo na Mkuu wa Kikosi cha Kambi ya Jeshi ya Kizumbi, Luteni Kanali Mussa Kingai, mara baada ya wanajeshi hao kumaliza kufanya usafi wa mazingira pamoja na kutoa msaada wa chakula.
Kingai alisema kutokana na wimbi la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kuanza kushika kasi tena nchini, atahakikisha hakuna tukio lolote litakalowakumba watoto wanaoelelewa kituoni hapo.
“Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, tunalaani na kupinga matukio yanayotokea ya kuuawa kwa hawa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino), kutokana na baadhi ya watu kuendekeza imani za kishirikina, hivyo tunaahidi kuwahakikishia usalama dhidi ya watu hao,” alisema Luteni Kanali Kingai na kuongeza; “Pia tunaomba wananchi kutoa ushirikiano pale mbinu za kipelelezi zinapotumika na kuhakikisha wanafichuliwa wahalifu hao na mtandao mzima ili wachukuliwe hatua kali za kisheria kikiwamo na kifungo cha maisha ili liwe fundisho kwa watu wengine.”
Hata hivyo, Luteni Kingai alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu kwa jamii, ili waachane na mauaji hayo ya albino na wanawake wazee.
Kikosi hicho cha JWTZ Kizumbi kikiwa kinaelekea kuadhimisha Miaka 50 ya kuundwa kwa Jeshi hilo hapa nchini (1964), ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kesho Septemba Mosi mwaka huu, kilitoa msaada wa chakula, magunia mawili ya maharage na mahindi kituoni hapo.
Pia walitoa msaada wa sukari kilo 50, mafuta ya kupaka katoni mbili, mafuta ya kula ndoo mbili, kilo 25 za unga wa sembe, majani ya chai, chumvi, sabuni za kufulia na mbuzi wawili.
Akitoa shukrani kwa niaba ya watoto hao, Mlezi wa kituo hicho Zainabu Hussein alilishukuru jeshi hilo kwa msaada walioutoa na kuwasafishia mazingira, huku akitoa wito kwa jamii iachane na masuala ya imani za kishirikina yanayofanya kuibuka kwa mauaji. Kituo hicho cha Buhanghija kinalea watoto wenye ulemavu mbalimbali 270.
Wasioona 40, viziwi 52 na albino 178 ambao ndio walengwa wakuu wa mauaji na ukatili kutokana na imani potofu za kishirikina walizonazo baadhi ya watu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
aziz bilal00:49
1
Reply
Time muafaka kwa jeshi letu kuingilia hili suala
Post a Comment