Friday, 15 August 2014

AJIUNGUZA MWILI MZIMA KWA WIVU WA MAPENZI


Ajiunguza mwili mzima wivu wa mapenzi

MKAZI wa Igombe katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jijini hapa, Tausi Juma (22) amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kujimwagia mafuta ya taa na kujiunguza mwili mzima kutokana na wivu wa kimapenzi.


Tukio hilo ni la Agosti 9, mwaka huu saa 2 asubuhi nyumbani kwake. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime alipoulizwa, alisema ofisi yake haijapata taarifa juu ya tukio hilo.
Muuguzi wa zamu katika wadi hiyo, Pendo Muleta akizungumzia hali ya mgonjwa huyo alisema si nzuri, kwani ameungua asilimia 60 ya mwili wake.
Alisema mpaka sasa wanaendelea kumpatia matibabu ikiwemo dawa za kupunguza maumivu na zinazozuia maambukizo kutokana na vidonda alivyo navyo.
Mwanamke huyo akizungumza kwa tabu hospitalini hapo, alielezea kisa kwa kusema amefikia hatua hiyo baada ya kugundua mumewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.
Alidai mwanamke huyo alituma ujumbe kwenye simu ya mkononi ya mumewe na akauona.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika hospitalini hapo jana, Tausi alisema aliona hana umuhimu wa kuendelea kuishi na mtu ambaye anampenda kwa dhati, lakini anakuwa na mwanamke mwingine.
Akielezea alivyojiunguza, Tausi alisema wakiwa nyumbani kwao na mumewe aliyemtaja Hussein Yadunia ambaye ni polisi katika Kituo cha Polisi Igombe, wilayani Ilemela, jijini Mwanza, ujumbe wa maneno uliingia katika simu ya mume wake huyo.
Alisema hakumbuki maneno yote yaliyokuwemo kwenye ujumbe, lakini baadhi yalisomeka ‘nakupenda sana honey wewe ndio chaguo la moyo wangu.’
Mwanamke huyo alisema alipomhoji mumewe ambaye pia hujishughulisha na uvuvi wa samaki, juu ya ujumbe huo, alidai kutofahamu namba iliyotuma.
“Nilipomuuliza alikataa kuwa mtu huyo hamjui na aliniambia nimpigie simu…na mie nilipopiga simu hiyo ilipokewa na mwanamke kwa hasira nilimuuliza tena mume wangu ambaye alikataa tena kwa kuniambia hamjui,” alisema Tausi.
Huku akionekana kuwa na maumivu makali kutokana na sehemu kubwa ya mwili wake kuwa na majeraha ya kuungua, Tausi alisema ghafla mumewe alimbadilikia na kuanza kumgombeza kuwa amechoka na maswali yake na kumfuatilia kila siku maisha yake hivyo afungashe mizigo yake aende kwao.
“Baada ya maneno hayo, nilimuona mume wangu akiingia ndani na kuanza kunifungashia mizigo, akipakia nguo zangu kwenye mabegi nirudi kwetu na alifanya hivyo baada ya kumjua mwanamke aliyemtumia ujumbe wa maneno katika simu yake,”alisema.
Tausi ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa mumewe ndiye anayemhudumia hospitalini hapo, aliendelea kusimulia, “nilimwambia mume wangu kuliko kuondoka wakati bado nakupenda bora nijiue.”
Alisema moto mkubwa uliokuwa ukiwaka ulimshitua mumewe ambaye alimkimbilia na kumwagia mchanga na baada ya moto kuzimika alimvua nguo na kumkimbiza katika Kituo cha Afya cha Karume.
Kutokana na majeraha kuwa makubwa, iliamuliwa akimbizwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure ambayo pia ilimpa rufaa kwenda Bugando.
Hussein Yadunia ambaye ni mume wa mke huyo, akizungumzia tukio hilo alisema, “ Sina usemi.
Tayari tukio limetokea, yote namkabidhi Mungu lakini tukio hilo limenidhihirishia kuwa mke wangu ananipenda.”
Aliendelea kusema, “hata vyombo vikiwa kabatini huwa vinagongana lakini uamuzi aliofanya mke wangu umenishangaza.”
Akizungumzia ujumbe wa simu uliosababisha mtafaruku, alisema ulitoka kwa dadake na walikuwa wakitakiana heri. “Haikuwa meseji ya mapenzi,” alisema na kusisitiza akipona ataendelea kuishi naye na atazidi kumpenda.

1 comment:

Anonymous said...



aziz bilal04:01


1
Reply

Pole sana dada yangu kwani huyo mpenzi wako alikuwa anakupa kitu gani mpaka ukaamua kujiunguza na mafuta?

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!