Friday, 23 May 2014

POLISI WADAIWA KUFANYA UNYAMA DAR


PICHA HII HAIHUSIANI NA HABARI HUSIKA!
MKAZI wa Kigamboni, Baraka Mashauri (27) amedai kupigwa risasi katika mguu wake kulia na askari polisi wa kituo kidogo cha Gymkhana, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu tukio hilo, Mashauri alisema lilitokea Mei 17 mwaka huu, saa saba mchana akiwa katika mtaa wa Shaban Robert akipata chakula karibu na Mgahawa wa Holiday White akiwa na mwenzake aliyemtaja kwa jina la Musa Mohamed.


Mashauri alisema kuwa baada ya muda mfupi lilitokea kundi la watu wakimkimbiza mwizi ambaye alikamatwa na kupelekwa katika kituo hicho cha polisi.
Alisema kuwa baada ya hapo, walitokea askari watatu waliokuwa wamebeba silaha na walipomkaribia walimuita kwa jina lake kisha na kuanza kumpiga risasi.
“Walinirushia risasi, kwa kuwa pembeni kulikuwa na mwenzangu aliyejipumzisha, naye ilimpata ya pajani. Risasi ya kwanza niliikwepa na ndipo askari mmoja miongoni mwa wale watatu, Mohamed Shunda ambaye ni OCS, alinipiga risasi huku akiniuliza ile simu aliyoiba yule mwizi iko wapi.
“Wakati nikiwa nagaa gaa chini kwa maumivu, alikuja mtu akanieleza kuwa yule mwizi kasema alimpa simu mtu aliyekimbilia maeneo ya Gymkhana na baada ya hapo askari wale walinichukua kwa gari lao aina ya Defender na kuelekea kituo cha polisi cha Central, waliniacha kwenye gari na baada ya muda wakaja na fomu ya matibabu (PF3) na kunipeleka Hospiatali ya Muhimbili ambako waliniacha hapo huku wakiondoka na fomu hiyo,”alisema.
Mashauri aliongeza kuwa baada ya kufika Muhimbili alipata matibabu na kufungwa bandeji ngumu (POP) katika kidonda kilichotokana na risasi.
“Nilifikishwa saa 9 alasiri na nikatolewa Mei 18, lakini huu mguu kama unavyouona siwezi kutembea, ndani unauma nahisi kuna vitu na sijui hatma ya yangu itakuaje. Nimeandikiwa dawa ila fedha sina, ninadaiwa na hospitali sijui naishije,”alisema.
Katika kutoa malalamiko yake, alifika katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kuonana na mratibu wa kituo hicho aliyemtaja kwa jina la Mkuta Masoli.
Tanzania Daima limeiona picha ya Xray inayoonesha namna risasi hiyo ilivyopenya na kuvunja mfupa pamoja na uthibitisho wa vyeti vilivyotolewa vikiwa vimesainiwa na Dk. Stephen wa Taasisi ya Mifupa (MOI).
James Yustas, ambaye alimsaidia Mashauri kufika katika ofisi za gazeti, juzi alijikuta matatani baada ya kukamatwa na polisi na kupelekwa kituo cha kikuu na kuhojiwa sababu za kumpeleka mlalamikaji katika vyombo vya habari na ofisi za LHRC.
“Nilikamatwa juzi na askari wakaniweka rumande ambako walichukua simu zangu zote mbili lakini waliniachia jana saa moja asubuhi na kunitaka niachane na suala hilo,” alisema Yustas.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema hana taarifa nalo na hivyo kuomba waandishi kumsaidia kumkutanisha na majeruhi huyo ili aende akatoe maelezo yake.
Alisema “siwezi kuzungumza chochote kuhusu tukio hilo kwa sababu hakuna aliyefika kunilalamikia kuhusu tukio hilo, hivyo naomba kama mnajua alipo mwambieni aje kulalamika,” alisema.
TZ-DAIMA.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!