Thursday 29 May 2014

MCHAI CHAI NI ZAIDI YA KIUNGO

KINYWAJI cha chai huwa ni muhimu karibia kwa kila binadamu katika nyakati za asubuhi. Humfanya mtu kuchangamka na kuweza kufanya shughuli zake za siku.
Ni kutokana na umuhimu wa kinywaji hicho, wengine wasipopata huwa wanaumwa na kichwa.

Kama ilivyo kwa aina nyingine ya vinywaji na vyakula, chai nayo hunogeshwa na viungo mbalimbali ili kumpa raha zaidi mnywaji.
Viungo hivyo ni pamoja na mdalasini, iliki, tangawizi, pilipili manga na bila kusahau mchaichai.
Pamoja na kuorodhesha aina hizo za viungo, leo makala hii iliyotokana na mahojiano na mganga wa tiba mbadala, Abdallah Mandai, inaelezea kwa undani kuhusu mmea wa mchaichai ambao una kazi lukuki katika mwili wa binadamu.
Mandai anasema kuwa mchachai mbali ya kuwa kiungo kinachotumiwa katika chai, pia una faida tatu.
 Harufu nzuri
Mandai anasema kwa harufu iliyojaliwa mmea huu, ni wazi kwamba unaweza ukajikuta unakunywa chai yake bila ya kitafunio, na pia wakati chai hiyo ikishuka kwenye koromeo mnywaji hujisikia burudani.
Matibabu
Katika matibabu, anasema unatibu magonjwa yasiyopungua matano, ikiwemo kushusha joto, hasa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na malaria kali.
Mchaichai pia una kazi ya kusafisha figo ambayo kazi yake kubwa ni kusafisha damu mwilini, kuondoa mafuta mabaya mwilini ambayo mengi yanatengenezwa na kemikali kiwandani na hivyo mwili kushindwa kuziondoa na baadaye kusasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani.
Figo inapokuwa safi na imara, hata kazi nyingine kama kusafisha mkojo zinafanyika kirahisi kwani mkojo unapozidi kuwa mchafu mtu hujikuta akivimba mwili na wakati mwingine kufikia hata hatua ya kupoteza maisha.
Mchaichai pia huwasaidia kina mama ambao wanaumwa na tumbo kipindi cha hedhi, ambao wengi wao huchukulia kama chango.
“Unapokunywa mchaichai, unawezesha kusafisha mirija ya uzazi na hivyo kuwezesha damu kupita kwa urahisi,” anasema Dk. Mandai.
Anasema vilevile mchaichai una kazi ya kusafisha damu, hasa kwa watu ambao wamekuwa na tabia ya kupata magonjwa ya ngozi kama mapele na kutoka majipu.
Mchaichai pia unaelezwa kuwa ni dawa ya kuzuia kuharisha ambapo una uwezo wa kupambana na mdudu aina ya protozoa anayesababisha ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Mandai, utafiti uliofanywa mwaka 2009 na Chuo cha Gulioni cha nchini Israel, uligundua kuwa mchaichai una uwezo wa kuondoa seli zinazosababisha ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ni tishio kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Endapo mjamzito atatumia majani ya mmea huu kwa muda mrefu, ataweza kujiepusha kujifungua kwa njia ya upasuaji kwani husaidia katika kulegeza nyonga ambazo hubana katika kipindi cha ujauzito na kufanya njia kuwa ndogo kuwezesha mtoto kupita,” anasema.
Hata hivyo kwa wagonjwa wanaosumbuliwa hasa na vidonda vya tumbo, Mandai anasema mchaichai husaidia kuondoa gesi ambazo huwapata mara kwa mara.
Virutubisho mwilini
Kwa wagonjwa wa ukimwi, mchaichai unaelezwa kuwa huongeza CD4 na inashauriwa kuwa ni vyema mgonjwa wa aina hiyo akapendelea kutumia zaidi mchaichai kuliko majani ya chai.
Wito
Kwa kuwa tayari nchi nyingi za Ulaya na Asia zimekuwa zikitumia kiungo hicho kwa hali ya juu na kukipa kipaumbele katika suala zima la tiba, Mandai anasema imefika wakati sasa Watanzania wakajikita katika kilimo cha zao hilo.
“Unajua tayari soko lipo na itawezesha wakulima kujikwamua katika umasikini kwani kilimo chake hakihitaji gharama kubwa na ni mmea ambao unaweza kuota katika mazingira yoyote,” anasema Mandai

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!