Wednesday, 21 May 2014

MBWA AUA WATOTO WAWILI AMBAO NI NDUGU


Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Ester Shaban (44) amejikuta akirudia machungu ya kufiwa na mume wake kwa kufiwa na watoto wa kuwazaa kutokana na kuumwa na mbwa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Ester alifika Kibamba-Kwembe, nje kidogo ya Jiji la Dar na watoto wake watatu akitokea Kahama, Shinyanga ili kupumzika kwa ndugu yake baada ya kufiwa na mume wake miezi kumi na nne iliyopita.
Siku ya pili tangu afike watoto wake, Boniface Joseph (4) na Peter Joseph (6) waling’atwa na mbwa sehemu za usoni.
Tukio hilo lilitokea wakati mama yao amekwenda Makondeko, Dar na kuwaacha watoto hao nyumbani bila kuwepo kwa mtu mzima.
Chanzo kilisema mwanamke huyo alirudi saa mbili usiku na kukutana na mkasa huo wa watoto wake kung’atwa na mbwa, wakiwa na majeraha usoni.
“Mtoto mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema watoto hao ndugu waling’atwa usoni na mbwa wa mzee mmoja ambaye hata yeye alimkimbiza mchana,” kilisema chanzo hicho.
Naye mama wa mtoto  huyo akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa masikitiko, alisema: “Baada ya kukuta wanangu wamekumbwa na mkasa huo niliwachukua mpaka kwa mwenye mbwa na kumweleza lakini akakataa kwamba si mbwa wake japokuwa alionekana kuwa na kigugumizi cha hapa na pale.”

Akaongeza: “Tulishauriana tuwapeleke Hospitali ya Tumbi (Kibaha) lakini yule mzee aliyesemekana kuwa ndiye mwenye mbwa akasema yeye hana pesa za kukodi gari labda tusubiri Jumatatu. Siku hiyo ilikuwa Jumamosi tena saa tatu usiku.

“Nilipinga, ikabidi kesho yake (Jumapili) tuwapeleke hospitali ya binafsi ya Gati ambapo walichomwa sindano za tetenasi tu.

“Niliwauliza madaktari kama sindano hizo zinatosha wakasema zinatosha kwani chanjo niliyoipata mimi wakati wa ujauzito itawasaidia na watoto. Nilishangaa kwa sababu nasikia mtu akiumwa na mbwa anachomwa sindano za kitovuni lakini wanangu hawakufanyiwa hivyo.”

Mwanamke huyo aliendelea kudai kuwa daktari alimtoa wasiwasi kwa kumwambia vidonda hivyo vitapona asiwe na shaka. Akapewa dawa za kumeza watoto wake na kuruhusiwa kurudi nyumbani. 
Akasema: “Baada ya siku kadhaa, vidonda vilionekana kukauka kwa nje, Kumbe sikujua kwa ndani watoto wangu walikuwa wanaumia pasipo kufahamu. Siku chache mbele Peter akazidiwa.

Akawa anatapika damu na kubweka kama mbwa. Ila sikujua cha kufanya, kwa kuwa ilikuwa usiku nilivumilia.

“Ilipofika alifajiri ya saa 10 mwanangu alikata roho. Tulipeleka mwili kwenye mochwari ya Tumbi kwa ajili ya kuuhifadhi.

“Siku iliyofuata tukiwa mochwari tunauchukua mwili, tulimsimulia daktari ugonjwa uliomuua mwanangu akasema tumpeleke Boniface (mwanaye mwingine) ili afanyiwe matibabu. Kumbe kule nyumbani Boniface naye alikuwa amezidiwa na yuko njiani wanamleta hospitali. Alipofikishwa tu hakukaa sana akafariki dunia,” alisema mwanamke huyo.Mwanamke huyo akaendelea kusema kufiwa kwa watoto wake hao ni pengo kubwa sana katika maisha yake kwani kwa sasa amebaki na mtoto mmoja ambaye ni wa mgongoni.

“Moyo unaniuma sana ila sina namna zaidi ya kumshukuru Mungu kwa yote. Nilikuja kupumzika na watoto wangu hapa baada ya kifo cha baba yao, sasa siku nikirudi Kahama nitakuwa peke yangu,” alisema mama huyo na kuanza kulia.

Mwanamke huyo pia alisema anawaomba wasamaria wema wamsaidie kwa hali na mali kwani kwa sasa ni mjane na anahitaji kurudi Kahama ili kupeleka msiba wa watoto wake.

Kwa yeyote mwenye kuguswa na matatizo ya mama huyu anaweza kumsaidia kwa namba  0767 449758, jina litasoma Stella Shaban.

Marehemu hao walizikwa katika Makaburi ya Kibamba, Dar kwa kupishana siku moja. Mungu azilaze pema peponi roho zao. Amina

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!