Wednesday, 7 May 2014
HABARI ZAIDI KUHUSU BOMU LILILOLIPUKA NA KUJERUHI VIBAYA JIJINI MWANZA
BOMU limelipuka katika nyumba ya kulala wageni iliyopo katika eneo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Imani, jijini Mwanza na kujeruhi vibaya mtumishi wa kanisa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Rogart Mollel, alimtaja aliyejeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Bernadetha Alfred, ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Akizungumza kwa masikitiko, Katibu huyo alisema bomu hilo lililipuka juzi saa 2 usiku na kusababisha taharuki kubwa kwa wageni waliokuwa kwenye nyumba hiyo na watu wanaoishi jirani na kanisa hilo.
Kutegwa
Akifafanua zaidi kuhusu bomu hilo, Mollel alisema lilifungwa katika kifurushi kilichopambwa na karatasi za zawadi na kuwekwa katika mfuko uliotelekezwa katika korido ya nyumba hiyo kwa takribani siku tatu.
Kwa mujibu wa Mollel, eneo hilo la korido huwekwa kreti za soda na wageni wamekuwa wakiingia na kutoka kutumia njia hiyo, na wakati mwingine hupata chakula na chai katika eneo hilo, ndio maana watumishi hawakuhisi kwa haraka kama ni kitu cha hatari.
Kulipuka
“Jana (juzi) mhudumu huyo aliamua kufungua kifurushi hicho ili kuona ni nini na ndipo lilipomlipukia na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo usoni na miguuni na kukimbizwa Bugando kwa uchunguzi na tiba,” alisema Mollel.
Lakini Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Mkoa wa Mwanza, Askofu Zenobius Isaya, alielezea kwa undani kuwa Bernadetha aliamua kwenda kuchukua boksi hilo la zawadi juzi usiku, kwa kuwa lilikuwa limetelekezwa tangu Ijumaa iliyopita.
Kwa mujibu wa Askofu Isaya, nia ya Bernadetha ilikuwa kufahamu ni la nani na kwa nini lipo kwenye korido hiyo kwa muda mrefu, ndio kufungua likamlipukia.
Alipoulizwa kuhusu ulinzi uliopo katika eneo hilo la Kanisa Kuu la KKKT, Mollel alisema ulinzi upo katika mageti yote mawili lakini upekuzi huwa haufanyiki kwa kina.
“Kwa kweli tukio hili limetuchanganya sana, tumekuwa tukisikia matukio hayo yakitokea maeneo mengine makanisani, kwetu limetokea kwenye nyumba ya kulala wageni, sina hakika waliofanya hivyo walilenga nini,” alisema na kuongeza; “ tunashukuru Mungu haijaleta madhara makubwa sana.”
Mashuhuda
Baadhi ya watu waliohojiwa walidai waliposikia mlipuko huo, walidhani ni transfoma ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa kuwa mara baada ya kulipuka, umeme ulikatika katika eneo hilo.
Mlinzi aliyekuwa zamu siku ya tukio, Charles Mathayo, alidai baada ya mlipuko huo alisikia kilio cha mhudumu Bernadetha akiomba msaada, na walipofika walimkuta akiwa amelala chini akilia huku damu zikimtiririka huku kukiwa na misumari midogo midogo katika eneo hilo.
Shuhuda ambaye kwa wakati huo alikuwa amekaa nje kwenye ngazi, Elina Emmanuel, alidai alisikia mlipuko mkubwa na kuona moshi huku waliokuwa vyumbani wakianza kutoka nje.
Elina ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha kompyuta alidai alikuwa kwenye nyumba hiyo na baada ya mlipuko huo wageni walihamishiwa kwenye nyumba nyingine ya kulala wageni.
Polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentine Mlowola, alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo saa 2.20 usiku na kusema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.
Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa unaendelea kubaini nani aliyefanya kitendo hicho na kwa sababu gani, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ingawa mpaka jana hakukuwa na mtu aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo.
Kamanda Mlowola ametoa mwito kwa wananchi wanapoona vitu wasivyo na uhakika navyo na kuwa na wasiwasi navyo wasivishike, badala yake watoe taarifa Polisi.
Mganga Msaidizi wa Idara ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, aliyejulikana kwa jina moja la Baraka alisema kwa sasa waandishi hawaruhusiwi kumuona, kuongea wala kumpiga picha majeruhi kutokana na hali yake kuwa mbaya na kwa wakati huo hakukuwa na ndugu yake hata mmoja.
Imeandikwa na Grace Chilongola, Mwanza na Theopista Nsanzugwanko, Dar es Salaam
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment