WATU wanne wamefariki dunia kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji, na wengine tisa kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya Igunga, mkoani Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, alisema mapigano hayo yalitokea juzi, saa 7 mchana.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Chawala Doke, Mohammed Msengi, Biblo Kingu na Peter Karongo, wote wakazi wa Kijiji cha Isakamaliwa.
Kingu alisema watu wote waliohusika na mauaji hayo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Mbali na vifo hivyo, alisema nyumba 12 zimechomwa moto na kutokea uharibifu mkubwa wa mali za wananchi.
Pia alisema zaidi ya watu 20 hawajulikani walipo, huku wengine zaidi ya 150 wakiwa hawana makazi kutokana na nyumba zao kuchomwa moto kwenye mapigano hayo.
Alisema vitendo hivyo vimefanywa na wafugaji wanaoishi Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, pembezoni mwa Mto Manonga ambao umetenganisha wilaya hizo mbili.
Kingu alisema sababu za mauaji hayo ni wafugaji jamii ya Kitaturu kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima wa Wilaya ya Igunga pamoja na kugombea mpaka wa eneo hilo
No comments:
Post a Comment