HAWA wanaong’ang’ania kuishi mabondeni wachunguzwe kwa sababu huenda wakawa wana matatizo ya kiakili.Inabidi iwe hivyo kwa sababu haiwezekani matatizo yanayowakumba wakati wa mvua mara kwa mara, hurudi tena mvua inapopungua.
Kutokana na mazingira kama hayo, inanishawishi kuamini kuwa watu hawa wana matatizo ya akili, hivyo ni vema serikali ikawapima na kuwaondoa kwa nguvu kuwapeleka katika hospitali za wagonjwa wa akili.
Nguvu wanazopaswa kuzitumia serikali kipindi hiki ambacho mvua zimepungua, ni kuanzisha Operesheni Safisha, kwa kuzivunja nyumba zote katika maeneo hayo ya mabondeni.
Hili litekelezwe haraka kwa sababu haipendezi kuisikia serikali ikilalamika kila siku kwa kuwaomba wakaidi hao waondoke katika maeneo hayo.
Kitendo cha kuwabembeleza watu hao, ndicho chanzo cha kuendelea kuiletea aibu serikali kila kipindi cha mvua kinapowadia.
Mfano mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa, wakazi hao baada ya baadhi yao kunusurika kufa hivi sasa wamevamia vituo vya mabasi ya mradi wa magari yaendayo haraka kuvifanya makazi yao.
Kitendo hicho kinaonekana kuwakera baadhi ya wakazi wa jiji hadi kuitaka serikali kuwakamata watu hao na kuwafikisha mahakamani.
Madai ya kukamatwa wakazi hao wa mabondeni, baadhi yao wanadaiwa kuwa ni wale miongoni mwa waliopewa viwanja kule Mabwepande, lakini kutokana na nia yao mbaya viwanja hivyo wameviuza na kurudi tena katika maeneo hayo hatarishi.
Katika mazingira kama haya ya uendawazimu, haiingii akilini kwa watu hao kuonewa huruma kwa sababu wanayoyafanya ni sawa na kujitakia.
Ni kwanini watu hao wawe tayari kuishi katika eneo ambalo wanajua kuwa wakati wowote wanaweza kufa kutokana na mafuriko wakati wa mvua?
Mafuriko yaliyotokea hivi karibuni yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 10; nilidhani ingekuwa fundisho kwa wakaidi hao, lakini wapi, baada ya mvua hiyo kupungua juzi na jana wameanza kurudi tena katika maeneo hayo!
Kurejea kwao kwenye maeneo hayo ni dhahiri kuwa hawaheshimu kauli zinazotolewa na viongozi, zinazowataka kuondoka kwani serikali haiko tayari kuwasaidia katika matokeo yoyote watakayokabiliana nayo.
Watu hawa wanalitia aibu taifa kwa sababu mafuriko yalionekana dunia nzima kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, sasa ni wakati kwa serikali kulimaliza tatizo hili bila kumuonea aibu yeyote.
Nitashangaa kuona akajitokeza mtu kuwatetea watu wale. Kwa atakayefanya hivyo naye pia atakuwa na matatizo na hawatakii maisha mema.
Mtu anayefaa ni yule anayewashauri waache ukaidi wa kung’ang’ania kuishi katika maeneo hayo hatarishi.
Lakini kwa kuwashawishi kuwa watashinda kisheria waendelee kuishi katika maeneo hayo, ni sawa na kujionyesha mbele ya jamii kwamba hawajitambui.
Waelewe kuwa hata wakishinda kesi kuishi katika maeneo hayo, bado watakaokuwa karibu na kifo ni wao wakati wa mvua utakapowadia kama hivi sasa na wala sio sheria iliyowasaidia kuishi hapo.
Ni vema watu hao wakakaa chini na kufikiria ukaidi wanaoufanya wa kung’ang’ania maeneo hayo hatarishi wanamkomoa nani?
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment