Tuesday, 22 April 2014

TUSIWANYANYASE WATOTO WA MITAANI

HIVI sasa kuna wimbi la watoto wa mitaani katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambao hawana uangalizi  kama walivyo watoto wengine.
Ni fursa sasa kwa jamii kujiuliza inawasaidia vipi watoto hawa.

Watoto wa mitaani wana majibu mengi kuhusu maisha yao, tena wanavyo vilio vingi pamoja na ndoto pia lakini ni vipi zitatimia?
Wakati mwingine wanataka kupaza sauti zao wakitaka kuulizwa kwa nini wapo mitaani? Bahati mbaya hayupo wa kuwauliza bali wapo wa kuwanyanyapaa zaidi na zaidi.
Maisha ya watoto hawa ni hatarishi kupindukia kwa sababu hukumbana na matatizo makubwa na mabaya kwa afya, mwili na akili zao, hata wakiwa mitaani hukumbana pia na changamoto nyingi kutoka kwa watawala, vyombo vya dola na wanajamii wengine.
Lazima tubadilike tuwape nafasi na wao kueleza kero zao ili  tuzifahamu, kwasababu njia bora ni kujua chanzo cha tatizo, si kuangalia na kutibu dalili.
Kama tunakubali watoto ni hazina ya leo na ya baadaye, basi wanahitaji kutunzwa, kulindwa na kuendelezwa kwa kupewa elimu kwani hazina isiyotunzwa huharibika.
Labda malezi ya wazazi yanachangia uwepo wa watoto wa mitaani kuendelea kuwepo, hivyo kuharibu hazina na umuhimu wa mtoto.
Kwa hiyo dunia ifungue sikio lake na imsikilize mtoto na kumtambua. Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani badala ya kuwa darasani wana uwezo, maarifa na vipaji vya kipekee na wapo wa namna hii ambao wamefanikiwa katika mambo mengi baada ya kupatiwa fursa na jamii.
Ila watu wengi wamekuwa wagumu kuwaamini kwakuwa tumekwisha kuwanyanyapaa vya kutosha kwa kuwapa majina ya ajabu ajabu lakini pamoja na hayo wapo waliofanya na wanaoendelea kufanya maajabu makubwa katika nyanja nyingi baada ya kupatiwa fursa ya kuonyesha uwezo ama vipaji vyao.
Mathalani mtoto aitwae Hamisi ni bingwa wa dunia katika mchezo wa kuruka kamba huku timu ya watoto wa mitaani kutoka nchini kwetu wameshinda kombe la dunia katika mchezo wa mpira wa miguu.
Haya ni matokeo bora kabisa katika kuwapatia watoto hawa fursa. Hivyo hatuna budi kuwazuia wasiende mitaani ili wapate fursa zao wakiwa majumbani kwao.
Tukumbuke watoto ni hazina ya leo na baadaye fungua masikio uwasikilize, uwaone na uwape nafasi waweze kuondokana na maisha ya mitaani ambako wamekuwa wakikumbana na vitendo vya unyanyasaji, hasa nyakati za usiku.
Kutokana na hali hiyo pamoja sababu nyingine kumekuwa na ahadi za serikali zisizotekelezeka kwamba watawaondoa watoto hao katika mazingira hatarishi.
Mazingira hatarishi na mateso yamekuwa yakiwasababisha watoto kuwa sugu, tofauti na umri wao.
Usugu huo unasababisha watoto hao kuwa wahalifu, wezi, watumiaji wa dawa za kulevya na makahaba, kwa sababu tu wamekosa uangalizi kutoka kwa jamii inayowazunguka.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!