Tuesday 22 April 2014

TANZANIA NA KONGO(DRC) WAKUBALIANA KULINDA ZIWA TANGANYIKA

SERIKALI za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na marafiki wengine kutoa msaada wa hali na mali katika juhudi za nchi hizo kutekeleza mradi wa Lukuga.

Wito huo ulitolewa na Waziri wa Maji wa Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe na mwenzake wa DRC, Bruno Kapandji Kalala, ambaye anaongoza Wizara ya Maji na Umeme.
Mawaziri hao walitoa wito huo walipokutana mjini Dodoma hivi karibuni kuzungumzia jinsi nchi hizo zinavyoweza kulinda rasilimali za Ziwa Tanganyika.
Mradi wa Lukuga unahusisha kujenga ukuta katika Mto Lukuga ambao ndio pekee unaotoa maji kutoka Ziwa Tanganyika, ili kuzuia upungufu wa maji katika ziwa hilo unaoshuhudiwa hivi sasa.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na maofisa waandamizi wa serikali zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya mawaziri hao, mkutano huo ulilenga kuweka mikakati ya pamoja na kutekeleza mapendekezo ya marais wa nchi hizo kuhakikisha ukuta unajengwa kwa haraka katika mto huo.
Mto Lukuga ndio pekee unaotoa maji kutoka ziwa hilo na kumwaga maji yake katika Mto Congo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pamekuwa na athari kubwa kutokana na kupungua maji ya Ziwa Tanganyika hasa katika miji ya Kigoma/Ujiji na Bandari ya Kigoma kwa upande wa Tanzania na bandari za Kalemie, Uvira na Moba kwa upande wa DRC.
“Panatakiwa ushirikiano wa nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika ili kushughulikia matatizo haya,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa mawaziri hao, kutekelezwa kwa mradi wa Lukuga ni hatua muhimu katika kutatua tatizo la kupungua maji katika ziwa hilo. Inatarajiwa kuwa mradi huo utagharimu dola milioni 65.
“Tumezingatia changamoto ya kupungua maji katika ziwa na athari zake kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya nchi zetu,” walisema mawaziri hao katika taarifa hiyo.
Ziwa Tanganyika linatumiwa na nchi nne ambazo ni Burundi, DRC, Tanzania na Zambia.
Burundi inamiliki asilimia 8 ya ziwa hilo; DRC (asilimia 45); Tanzania (asilimia 41); na Zambia (asilimia 6).  Tanzania na DRC zinamiliki asilimia 86 ya ziwa kwa pamoja.
“Tumedhamiria kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali ya ziwa hili yanakuwa endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” ilisema taarifa hiyo.
TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!