HATIMAYE Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu la Katiba imeridhia wajumbe wake kukatwa posho ya siku moja ambayo ni sh 70,000 kila mjumbe ili kuwasaidia waliokumbwa na mafuriko, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza kabla ya kuahirisha Bunge hilo, Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan, alisema jumla ya fedha zote ni sh milioni 44.
Alisema fedha hizo zitapelekwa ili kuisaidia serikali kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na watu walioathirika.
Aprili 15, mwaka huu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, alitoa hoja ya kuwaomba wajumbe 629 kuchangia posho japo ya siku moja kwa ajili ya kusaidia familia zilizokumbwa na maafa.
Waziri huyo alisema kitendo cha wajumbe kukubali kutoa posho hiyo kitadhihirisha umoja na mshikamano wao.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ameahirisha mkutano wa bunge kwa ajili ya kupisha Sikukuu ya Pasaka hadi Jumanne ya Aprili 22, mwaka huu.
Akiahirisha mkutano huo aliwataka wajumbe kuhakikisha wanachukua karatasi za bango kitita zenye maoni ya wengi na wachache ili wasome kipindi hicho cha mapumziko
TANZANIA DAIMA..
No comments:
Post a Comment