Tuesday 1 April 2014

DPP AWARUDISHA KIZIMBANI "WAFUNGWA WA MAGUFULI

Wafungwa wawili raia China waliokuwa wakitumikia kifungo cha miaka 20 kwa kosa la uvuvi haramu katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania (Exclussive Economic Zone- EEZ), maarufu kama wafungwa wa Samaki wa Magufuli, wamefunguliwa upya mashtaka.
Wafungwa hao, Hsu Chin Tai, ambaye alikuwa nahodha wa meli ya Tawaliq iliyokamatwa ikifanya uvuvi huo haramu, na aliyekuwa wakala wa meli hiyo, Zhao Hanquing, waliachiwa huru na Mahakama ya Rufani Ijumaa iliyopita.
Hata hivyo, jana walipandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa upya mashtaka ya awali yaliyowapeleka gerezani.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwarudisha tena kizimbani na kuwasomea upya mashtaka hayo baada ya Mahakama ya Rufani kutengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyowatia hatiani awali, kutokana na kasoro za kisheria katika kuwashtaki.
Katika hukumu yake, Mahakama ya Rufani ilisema mwenendo wa kesi hiyo katika Mahakama Kuu ulikuwa batili kutokana kosa walilolifanya kutokusikiliza hoja za upande wa utetezi kuwa washtakiwa walifunguliwa mashtaka hayo bila kibali cha DPP.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilitoa nafasi nyingine kwa DPP kuwafungulia upya mashtaka hayo kwa kufuata utaratibu kama angependa kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Hatua ya DPP kuwarudisha kizimbani tena Wachina hao na kuwasomea mashtaka hayo inamaanisha kuwa kesi hiyo inaanza upya tangu hatua ya kwanza, kama vile walikuwa hawajawahi kushtakiwa kwa makosa hayo.
Katika kesi hiyo mpya namba 13 ya mwaka 2014 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Warialwande Lema, washtakiwa hao walisomewa mashtaka mawili yanayowahusu wote kwa pamoja wakati mshtakiwa wa pili Hanquing akikabiliwa na shtaka moja zaidi.
Washtakiwa hao jana walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila akisaidiana na mawakili wengine wa Serikali Tumaini Kweka, Hamidu Mwanga na Rose Chilongzi.
Katika shitala la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya shuguli za uvuvi katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kibali, kinyume cha kifungu cha 18 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi Katika Kina Kirefu cha Bahari.
Wakili Mwangamila alidai kuwa Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009, washtakiwa hao kwa pamoja walifanya shughuli za uvuvi katika eneo la Tanzania bila kuwa na leseni.
Katika shtaka la pili wanadaiwa kufanya uchafuzi wa maji na mazingira ya bahari eneo la Tanzania kinyume cha Kanuni (1) (2) na kanuni ya 70 ya Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi katika kina kirefu cha bahari mwaka 2009

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!