Monday, 14 April 2014

DAR ES SALAAM YATENGWA!

 
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini mbali na kusababisha vifo na maafa mengine, zimeutenga Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi baada ya madaraja muhimu katika barabara zinazoingia kukatika.
Kutokana na athari za mvua hizo, njia kuu za kuingia Dar es Salaam, ikiwamo barabara za Morogoro, Bagamoyo na Kilwa zilifungwa jana na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri.
Maeneo yaliyoharibika ni karibu na Daraja la Mto Ruvu lililofurika maji na kusababisha magari kwenda mikoa ya Kaskazini, Magharibi na Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani kukwama.
Ukiacha barabara, safari za anga nazo ziliathirika kwa muda kuanzia mwishoni mwa wiki kutokana na barabara za ndege kutua na kurukia kujaa maji kutokana na mvua hizo zilizoambatana na upepo mkali.
Abiria wanaosafiri kwenda mikoani na nchi jirani walikwama katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Barabara ya Morogoro
Rais Jakaya Kikwete alitembelea eneo ya Ruvu Darajani na kukutana na maelfu ya wasafiri waliokwama kutokana na mafuriko. Aliwapa pole na kuahidi kuwa Serikali itapambana kurekebisha uharibifu huo.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliyewasili mchana akiambatana na mkewe, Mama Salma alisema: “Serikali ina uwezo wa kuzuia mambo mengine lakini haina uwezo wa kuzuia mafuriko na kinachotakiwa ni kumwomba Mungu ili hekima zake zifanye kazi na kuepusha hali ya hatari kwa wananchi.”
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliwataka wamiliki wa magari makubwa yaliyoko Dar es Salaam kusitisha safari hadi hapo hali itakapotengamaa.
Katika Mto Mzinga unaotenganisha Dar es Salaam na mikoa ya Lindi na Mtwara, ilibidi magari yazuiwe kuvuka baada ya daraja lilipo kati ya Mbagala na Kongowe kumegwa upande na mvua. Jana abiria walikuwa wakivuka taratibu katika upande uliosalia, lakini baadaye lilizolewa kabisa.
Kabla ya daraja lote halijazolewa na mvua, waandishi wetu walishuhudia mamia ya wasafiri wenye mizigo wakivuka katika daraja hilo huku wakiongozwa na polisi ili kupita.
Baada ya polisi kuona daraja hilo linazidi kubomoka, waliwazuia watu na baada ya muda mfupi likazolewa na maji
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!