ZAIDI ya wananchi 16,828 wa Mkoa wa Rukwa wamesaini ombi la haki (petition), wakiiomba Serikali kutenga bajeti mahususi ili kuviinua vituo vya afya nchini viweze kutoa huduma za dharura kwa za uzazi ikiwemo upasuaji, damu salama, vifaa vya kutosha na wafanyakazi wenye ujuzi.
Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama, Bi. Rose Mlay jana mjini hapa mbele ya mgeni rasmi wa siku ya Utepe Mweupe ambaye ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Seif Rashid aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.
“Lengo ni kuhakikisha bajeti ya kutosha inatengwa na Serikali Kuu pamoja halmashauri ili kuhakikisha kuwa angalau asilimia 50 ya vituo vya afya nchini vinatoa huduma za dharura za uzazi,” alisema Mlay.
Kwa Upande wake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika ujumbe wake ameziagiza mara moja halmashauri zote nchini kutenga bajeti ya kutosha ili kuimarisha vituo vya afya viweze kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwamo upasuaji lengo likiwa ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Tamko hilo lipo katika hotuba ya Waziri Pinda iliyosomwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid akimwakilisha Waziri Mkuu. Katika maelezo yake Waziri Pinda alisema vifo vya mama na mtoto baado ni changamoto nchini hivyo Serikali ina kila sababu ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Aliongeza kuwepo kwa huduma hizo na watalaamu kwenye vituo vya afya na hospitali nchini, ni njia pekee itakayosaidia kupunguza vifo hivyo.
“Kila mwaka karibu wanawake milioni sita hupoteza maisha ulimwenguni kote wakati wa kujifungua, asilimia 50 ya wanawake hawa wanatoka kusini mwa Jangwa la Sahara na Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizo kwenye ukanda huu.”
No comments:
Post a Comment