Thursday, 27 March 2014

TUACHE KUJADILI HOTUBA ZA KIKWETE, WARIOBA TUBORESHE RASIMU

Wiki ya Machi 18 - 22, 2014, mwenyekiti Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Bunge la Katiba.
Wiki hiyo iliishia siku ya Ijumaa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete alitoa hotuba kwa Bunge hilo Maalumu.
Hotuba zote zilipokelewa kwa hisia tofauti kulingana na msimamo wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa kuliko zote katika Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya, hususan suala la Muundo wa Muungano.
Wale wanaoshabikia muundo wa serikali tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba na wanaoshabikia muundo wa serikali mbili, walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Mimi Sikufurahishwa na hotuba zote mbili kwa sababu zifuatazo;
Hotuba hazikunifurahisha
Moja, hotuba zote mbili zilichukua muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita inayohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu suala hilo pekee.
Ni dhahiri kwamba suala hili ni kubwa na muhimu, kwani linahusu uhai wa dola yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo, masuala kama Haki za Raia ni muhimu zaidi kwani hata uwe na muundo wa namna gani wa Muungano au hata Muungano wenyewe kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia, katiba hiyo itakataliwa na wananchi.
Huu mtindo unaozuka wa kudhani muundo wa Muungano ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu, utatufikisha pabaya na hata kurudi tena kuandika katiba kwa lengo la kudai haki hizo. Jaji Warioba na Rais Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi hicho na kutambua kuwa Katiba ni zaidi ya Muungano.
Pili, Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu miundo ya Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana na misingi ama ya ‘malalamiko’ au ‘hofu’.
Jaji Warioba aliorodhesha malalamiko 11 ya upande wa Zanzibar dhidi ya Muungano na malalamiko kumi ya upande wa Bara. Kimsingi malalamiko yote ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo vya upande wa Zanzibar, isipokuwa lalamiko namba ‘vii’ linalohusu kupotea kwa utambulisho wa Tanganyika katika Muundo wa Muungano.
Jaji Warioba anajenga msingi wa pendekezo la tume yake kutokana na kujibu malalamiko au maarufu kama kero za Muungano na anasema “Muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa... waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye serikali mbili, na siyo nchi mbili zenye Serikali Mbili”. Nukuu hii niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu Warioba.
Rais Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye hofu za kuwa na serikali tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za kuendesha Muungano, kuzuka kwa hisia za utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari, uwezekano wa Muungano kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi kuchukua nchi ikibidi na kutupilia mbali katiba na Serikali ya Muungano kutokuwa na Rasilimali zake.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!