
Bosi Mkuu wa Simba anayemaliza muda wake, ametangaza kutogombea tena nafasi uenyekiti katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo kongwe yenye umri wa babu mwenye wajukuu wasiohesabika na vitukuu kibao. Uchaguzi utafanyika Mei mwaka huu.
Rage anaondoka Msimbazi akiwa na kapu la misuguano ya uongozi kati yake na baadhi ya wanachama, ambao mara mbili walitangaza kumtimua kupitia mfumo wa kizamani (mapinduzi). Shukrani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kukataa kubariki mapinduzi.
Kwa tathmini yangu binafsi, uongozi wa Rage katika klabu ya Simba naufananisha na mtu aliyenunua gari linalotumia muda mwingi kufanyiwa matengenezo gereji kuliko kutembea barabarani.
Maana yake nini? Kwamba, miaka minne ya Rage akiwa Simba imekuwa yenye misuguano na migogoro kuliko kinyume chake (furaha). Ni yeye ambaye muda mwingi aliutumia kuwatuliza wananchama wake waliokuwa wakimpinga.
Hakuwa na muda mwingi wa kufikiria maendeleo ya klabu, migogoro na misuguano ndiyo yalikuwa mambo ya kawaida kuyasikia kwenye vyombo vya habari.
Na ndiyo maana sishangazwi na kauli alizokuwa akizitoa kwenye mikutano kadhaa ya Simba, ukiwamo wa hivi karibuni kwamba anaondoka Simba kwa vile hana njaa wala yeye siyo maskini.
Namnukuu: “Mimi sitagombea...mimi siyo maskini, sina njaa, hata mkizomea nasema mimi sina njaa, na wanachama wengi mliopo hapa (Simba) ni mambumbumbu.” Kauli aliyoitoa kwenye mkutano wa hivi karibuni.
Niseme tu kwamba, sikutegemea Rage kama mwanamichezo wa kweli kutoa kauli kama hii ambayo ni kinyume na utamaduni wa ‘Fair Play’ kwenye mchezo wa soka.
Viongozi wanahitaji kuwa wavumilivu kwa wanaowaongoza na kuwa makini na kauli wanazotoa. Kwa tafsiri yangu, kauli ya Rage imejaa ubabe na majivuno yasiyo na tija kwa Simba.
Unaweza kuipanua zaidi kauli ya Rage katika taswira kwamba, wakati anagombea uongozi alikuwa maskini na mwenye njaa, lakini baada ya miaka minne anatufunua na kusema hana njaa wala yeye siyo tena maskini!
Kuwaita wanachama wa Simba mbumbumbu, ni udhalilishaji uliokosa kipimo. Wanachama hao ndiyo waliomchagua na kumwondolea njaa. Ndiyo hao waliomvumilia muda wote pamoja na kushindwa kutekeleza ahadi zake nyingi.
Hata hivyo, Rage amewaonya wanachama wa Simba kutofanya makosa katika uchaguzi ujao. Wasifanye makosa kuchagua viongozi ambao, muda wa kuondoka madarakani utakapowadia watawadhalilisha na kuwaita mbumbumbu.
MWANANCHI.
MWANANCHI.













No comments:
Post a Comment