Wednesday, 26 March 2014

MTUHUMIWA WA MENO YA TEMBO AJIDHAMINI MAHAKAMANI

Mtuhumiwa anayeshtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, ameruhusiwa kujidhamini mwenyewe, Mwananchi limebaini.
Rebeca Julius Mwita (32) anakabiliwa na mashtaka matatu ya kukutwa na nyara hizo za Serikali zenye uzito wa kilo 46 zikiwa na thamani ya Sh39.5 milioni aliruhusiwa kujidhamini mwenyewe kinyume cha kifungu cha  148 (5)(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.  Mwita alikamatwa Januari 17, 2013 na alifikishwa mahakamani siku nne baadaye, Januari 23 ambako alifunguliwa mashtaka manne ya kukutwa na meno ya tembo mawili na vipande vinne vya meno hayo, kinyume cha sheria.
 Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Amon Kahimba, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anesius Kainunura alidai kuwa makosa yanayomkabili mshtakiwa ni kinyume cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya 2009 kifungu cha 4(d) jedwali la 1 na Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho 2002.
 Baada ya kusomewa mashtaka, mtuhumiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana hivyo alirejeshwa rumande hadi Februari 4, 2013 wakati kesi yake ilipotajwa kwa mara ya pili.    Masharti aliyopewa ni kujidhamini mwenyewe kwa ahadi ya maneno ya Sh1 milioni, kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alipaswa kuweka bondi Sh2 milioni na sharti la tatu lilikuwa ni mdhamini mmojawapo kuwasilisha fedha taslimu Sh18 milioni.
Kesi hiyo iliendelea kutajwa bila mtuhumiwa kupata dhamana hadi Julai 9 na 23, 2013 wakati  wadhamini wawili ,akiwamo mume wake walijitokeza kumdhamini, lakini walishindwa licha ya kwamba wakati huo masharti yalikuwa yamelegezwa.
 Tofauti na masharti ya awali, kila mdhamini alitakiwa kutoa ahadi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh2 milioni pia mshtakiwa kujidhamini kwa fedha ya maandishi Sh500,000.
 Hakimu Kahimba aliwakataa wadhamini hao kwa maelezo kwamba hawakuwa na sifa, hivyo kuamuru mtuhumiwa arejeshwe rumande hadi Agosti 14, mwaka jana na kesi hiyo namba Eco.03/2013, ingetajwa kisha kusomwa kwa maelezo ya awali.
Dhamana ya ghafla
Katika hali isiyo ya kawaida, Julai 23, wakati waendesha mashtaka, karani na yeye (hakimu) akiwa ameshaandika tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo,  aliamuru shauri la mshtakiwa huyo lisomwe upya mahakamani.
 Uchunguzi umebaini kuwa baada ya shauri hilo kusomwa upya, Hakimu Kahimba aliruhusu Mwita ajidhamini mwenyewe kwa ahadi ya maandishi ya Sh500,000 na kuamriwa kufika mahakamani Agosti 14, 2013.
 Akizungumza na gazeti hili, Hakimu Kahimba alisema alitumia busara zaidi katika uamuzi wake, kutokana na mshtakiwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu kwa kukosa wadhamini.
 “Mshtakiwa pamoja na kuomba alegezewe masharti ya dhamana...Bado alishindwa, kutokana na kukaa muda mrefu na uhakika wa kumpata upo....Wakati mwingine tunatumia hekima zaidi,” alisema Kahimba
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!