Tuesday, 18 February 2014

WIMBO HUU WA "KULALAMIKA" HAUUZIKI

Kuna tatizo moja kubwa la viongozi wetu wa vyama vya michezo. Kulalamika. Kulalamika ndiyo utumwa wa viongozi hao. Kila siku habari ya vyama kukosa fedha ndiyo kiini cha mazungumzo.
Rais Jakaya Kikwete aliwahi kukinanga Chama cha Riadha Tanzania, akisema hakiishi kulalamika kila siku. Ukata, ukata ndiyo wimbo wa chama hiki. Kikwete alisema viongozi wanaolalamika kila kukicha kuhusu masuala la fedha, hawajui wajibu wao.
Naamini kuwa kiongozi mwenye dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi siyo kazi rahisi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati fulani aliwahi kusema kuwa anashangazwa na watu wanaotumia kila njia kwenda Ikulu.
Namnukuu: “Ikulu siyo sehemu ya kukimbilia. Ikulu ni mzigo, ukipita njiani unaona watu wanaomba, unaona watu wengi maskini, unahisi yote hayo ni mzigo wako kama kiongozi wa nchi.”
Yanayotokea nchini katika nafasi mbalimbali za uongozi, kuanzia siasa mpaka michezo ni kwamba tuna viongozi wasio na dhamira ya dhati ya kujitolea na kujituma kuwatumikia wananchi.
Viongozi wetu wanataka madaraka bila kujua nini watakwenda kufanya kama watawala. Katika hali kama hii, viongozi wetu hawawezi kubeba mzigo wa matatizo ya wananchi na badala yake wanakuwa sehemu ya kuongezeka kwa matatizo kila kukicha. Hawaishi kulalamika, wanalalamika hata pale ambapo hawakustahili.
Tanzania inajianda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola Julai mwaka huu Mjini, Glasgow, Scotland. Kimsingi, washiriki wetu walipaswa kuwa wanaendelea na mazoezi na siyo kujiandaa kuanza mazoezi. Kama kawaida, viongozi wao wameshaanza kuzungumza. Mazungumzo yao ni malalamiko.
Wimbo wao ni ukata. Hawawezi kujiandaa vizuri kwa sababu hawana fedha. Ni kweli, maandalizi yanahitaji fedha na wao fedha hawana kama wanavyolalamika na bado wanataka kwenda kushiriki.
Inashangaza kweli. Mashindano haya huja baada ya miaka siyo chini ya minne. Kwamba, walikuwa na muda wa kutosha kujipanga kutafuta fedha za maandalizi kama viongozi. Kipindi chote hawajafanya hivyo.
Wanabaki kusema wenzetu wamejiandaa vizuri, watafanya vizuri kwenye mashindano, kwa nini msiwe nyinyi? Mmekosa nini mpaka kuwapa sifa wenzetu kila siku?
Kwa hali ilivyo, Tanzania haiwezi kurudi na medali hata kama itapeleka wanamichezo 200. Medali waipate wapi wakati viongozi wa michezo wanatumia muda mwingi kulalamika badala ya kutafuta fedha za maandalizi.
Kama tunataka kujenga taifa lenye mafanikio katika michezo, kwanza ni lazima kuondokana na utumwa wa kuendelea kuwa na viongozi wa aina hii. Viongozi wanaokimbilia madarakani ili kuendeleza wimbo wa ‘Kulalamika’
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!