Tuesday, 18 February 2014

WAJUMBE WAWEKE MBELE UTAIFA, BUNGE LA KATIBA

Mjumbe wa Tume ya Katiba,Christopher Mtikila.PICHA|MAKTABA 

Leo Tanzania inaanza safari ya kuandika historia mpya ya kupata Katiba iliyotokana na Watanzania wenyewe, safari hiyo itachukua siku 70 na kama italazimika kuongezwa, zitaongezwa 20 kukamilisha kazi hiyo.
Waliopewa dhamana ya kufanya kazi hiyo ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linalojumuisha Wabunge na Wawakilishi 437, wajumbe wengine kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali (20), taasisi za kidini (20), vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu (42), taasisi za elimu (20), watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowakilisha wavuvi (10), vyama vya wakulima (20) na vikundi vya watu wenye malengo yanayofanana (20).
Macho na masikio ya Watanzania pengine na jumuiya ya kimataifa, yameelekezwa Dodoma ambako leo mchakato wa kuanza kwa kazi hiyo unaanza.
Tangu kutangazwa kwa Rasimu ya pili ya Katiba Mpya, Desemba 30, mwaka jana, viongozi mbalimbali wametoa nasaha mbalimbali kwa wajumbe wa Bunge hilo wakitaka wazingatie misingi ya utaifa katika kutuvusha kwenye hatua hii muhimu.
Katika nasaha zake, Rais Jakaya Kikwete aliwataka wajumbe hao watambue kuwa wana dhamana kwa Watanzania na taifa kwa jumla, hivyo anatarajia Katiba itakayoundwa itadumu kwa zaidi ya miaka 50.
Aliwataka wajumbe hao kuhakikisha Katiba itakayoundwa inaimarisha Muungano, amani, utulivu, mazingira mazuri ya kisiasa na uchumi na watangulize masilahi ya taifa.
Aidha, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutokutumia ubabe na jazba kuwasilisha hoja zao, bali kuongozwa na hekima katika kujenga hoja ili waungwe mkono.
Aliwaambia ili kupata Katiba tunayoitaka, lazima wajumbe watofautiane kwa hoja na ile inayoonekana kuwa na mashiko ndiyo ipewe nafasi kwa masilahi ya taifa na si watu binafsi au taasisi wanazotoka. Alitoa rai kwa wajumbe kuhakikisha mjadala wao usiwe na lengo la kuvunja au kudhoofisha Muungano, bali kuuimarisha.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amewataka wajumbe hao kutokukubali kununuliwa kwa chai wala fedha na kusahau jukumu lao la kulinda masilahi ya taifa.
Amewadokeza kwamba kuna vikundi ambavyo vimejiandaa kuhakikisha vinapenyeza mambo yao hivyo wanapaswa kuwa makini navyo.
Alisema wasishangae kuitwa kunywa chai mara kwa mara hata kama hawana njaa na kuitwa kula na kwamba wapo watakaojaribu kutoa hadi bahasha na kuwataka wajitambue na wasikubali kutumiwa.
Aliwaeleza kwamba busara kama zile za Mfalme Suleiman zinahitajika miongoni mwao, ili waweze kutambua kwa kina umuhimu wao katika kusimamia masilahi ya taifa wakati wanapokuwa wanachangia hoja zao kwenye Bunge la Katiba
MWANANCHI..

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!