Taarifa za takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyotolewa kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, inaonyesha wananchi 2,660 walitoa maoni kuhusu umri wa Rais.
Wananchi 1,428 ambao ni sawa na asilimia 53.7, walipendekeza umri wa Rais upunguzwe kutoka umri wa sasa wa miaka 40, asilimia 9.2 wakitaka ubakie kama ulivyo na asilimia 7.3 uongezwe.
Hata hivyo, haieleweki vigezo vilivyotumiwa na tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutozingatia maoni ya wananchi walio wengi kama ilivyofanya katika muundo wa Muungano.
Takwimu za Jaji Warioba zinaonyesha kwamba wananchi waliotoa maoni kwa upande wa Tanzania Bara katika suala la muundo, walikuwa watu 39,000 huku Zanzibar wakiwa 38,000.
Jaji Warioba alimweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa kati ya waliotoa maoni hayo Tanzania Bara, asilimia 60 walipendekeza Serikali tatu, asilimia 24 walitaka Serikali mbili na asilimia 13 walipenda Serikali moja.
Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 ya wananchi waliotoa maoni yao walipendekeza muundo wa Serikali mbili, asilimia 0.1 Serikali moja na asilimia 60 walipendekeza muundo wa Muungano wa mkataba.
Ibara ya 39 ya Katiba ya sasa inataka mgombea urais awe ametimiza umri wa miaka 40 wakati ibara ya 79(1) ya rasimu ya Katiba Mpya inapendekeza mgombea urais awe na umri usiopungua miaka 40.
Takwimu hizo zimepatikana wakati kukiwa na vuguvugu la wabunge vijana kutajwa kama watu wanaofaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Miongoni mwa wanaotajwa sana ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zuberi Zitto na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.
No comments:
Post a Comment