Monday, 24 February 2014

BALOZI KAZAURA AFARIKI DUNIA AKITIBIWA INDIA

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura amefariki dunia juzi, Chenai, India alikokwenda kwa ajili ya matibabu.
Rais Jakaya Kikwete alielezea kushtushwa na kifo hicho na kwamba alikuwa mtumishi hodari, mwaminifu, mwadilifu na kwa nchi yake.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDSM, (Utawala), Profesa Yunus Mgaya alisema kwamba uongozi wa UDSM utatoa taarifa rasmi leo.
“Ni kweli tumepata taarifa za kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Kazaura, uongozi utatoa taarifa rasmi kesho (leo),” alisema Mgaya.
Alisema Balozi Kazaura alikwenda India kwa matibabu kwa mara ya kwanza mwaka jana na alirejea nchini baada ya kupata nafuu.
Mgaya alisema Februari 13, mwaka huu alirudi tena India kwa ajili ya matibabu hadi kifo chake kinatokea.
Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala alisema chuo kimepoteza kiongozi ambaye alikuwa mfano wa kuigwa katika uongozi wake.
Oktoba 18, 2011, Balozi Kazaura aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mkuu wa Chuo cha UDSM katika kipindi kingine cha miaka minne,baada ya kumaliza kipindi kama hicho.
Kazaura aliteuliwa baada ya kifo cha Paul Bomani ambaye alikuwa mkuu wa chuo hicho tangu mwaka 1993 hadi alipofariki mwaka 2005.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!