Friday, 7 February 2014

RAIS KIKWETE KUTANGAZA BUNGE LA KATIBA LEO



RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajia kutangaza majina ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba. Akizungumza na viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa mjini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema kazi ya kuchagua wabunge wa Bunge hilo imekamilika na sasa wanamalizia changamoto ndogo ndogo zilizopo.

Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuweka usawa wa jinsia, pamoja na kuangalia iwapo wajumbe wa mkoa mmoja wamezidi.

“Wajumbe ambao hawatakuwepo katika majina 201 yatakayotangazwa kesho (leo), wasisononeke kama hawana sifa bali nikutokana na sababu mbalimbali,” alisema Kikwete.

Alisema alipokea majina 3,774 na baada ya kuchambua 3,753 yaliachwa.


Alisema kutoka kwenye taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), ambazo zina nafasi 20, yalipelekwa majina 1,647, taasisi za dini nafasi 20 alipokea majina 329, vyama vya siasa nafasi 42 yalipelekwa majina 198.

Alisema katika taasisi za elimu, nafasi 20 yalipendekezwa majina 130, wafanyakazi 19 walipendekeza 202, walemavu 20 walipendekeza 140, wafugaji 10 walipendekeza 47, wavuvi 10 walipendekeza 57, wakulima 20 walipendekeza 157, makundi ya mlengo unaofanana 20 walipendekeza 727.

Kikao cha kwanza cha Bunge la Katiba, kinatarajia kuanza rasmi Februari 18, mwaka huu kwa kuchagua viongozi wa Bunge hilo, kuapishana na baadaye kuzinduliwa rasmi.

Kikao hicho kitakaa kwa siku 70 na kuongezwa siku 20, ikiwa muda huo hautatosha kujadili rasimu ya pili ya Katiba Mpya.

Aliwataka wajumbe wa bunge hilo, kuweka utaifa mbele kwa kujua kinachopendekezwa na kupambanua kinachofaa kwa maslahi ya taifa.

“Hatua ya Bunge la Katiba ni tofauti na hatua zote zilizopita, sasa ni kutunga Katiba na siyo kutoa mapendekezo kama ilivyokuwa awali, jambo lisilofaa likipitishwa ni majuto ya baadaye,” alisema.

Kuhusu ukarabati wa ukumbi wa Bunge, Rais Kikwete alisema hadi kufikia Februari 10, mwaka huu kila kitu kitakuwa kimekamilika.

Alisema viti tayari vimepangwa na vipaza sauti vinaendelea kuwekwa, ikiwa ni pamoja na sehemu ya kurekodi kumbukumbu za kikao hicho.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray alisema katika vikao vya baraza hilo vimekubaliana kutotokea matusi na malumbano katika Bunge la Katiba, kama yaliyotokea katika vikao vya Bunge la kawaida.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema Katiba itakayoundwa sio ya CCM, Chadema, CUF wala chama chochote cha siasa na kama wabunge wakilitambua hilo, Bunge la Katiba litakuwa jepesi.

Aliwataka wanasiasa kuacha kwenda na mawazo yao katika bunge hilo, kwani itakuwa vigumu kufikia theluthi mbili.

Badala yake aliwataka wajadiliane kwa hoja na kusikiliza wengine ili kufikia muafaka.

“Kuwa na misimamo ya Katiba siyo vibaya, lakini ni vyema kujadiliana na kusikiliza hoja za wengine ili kufikia muafaka.

“Mtengeneze utaratibu wa jinsi ya kukwamua mambo yatakayokuwa na mivutano na siyo kuishia kutukanana, kwani ni vigumu kufikia theluthi mbili.

“Kama majadiliano yakiwa magumu, ni vema mkaahirisha kikao na kutoka nje kujadiliana na kisha kurudi kufikia muafaka.

Pia alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuangalia sheria ya kutenganisha biashara na siasa, ili kujenga misingi ya kimaadili kwa viongozi wa kisiasa

MTANZANIA.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!