Katika hali inayoashiria ukatili wa kutisha, wanaume watatu katika maeneo tofauti nchini, wamewaua wake zao kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Matukio hayo yametokea katika Wilaya za Chunya na Moshi na kuthibitishwa na makamanda wa polisi katika mikoa hiyo.
Makamanda hao walisema mauaji hayo yametokana na ugomvi wa wanandoa.
Katika tukio la Mbeya, polisi wamesema Agnes Daudi (32) mkazi wa Kijiji cha Shoga, aliuawa kwa kuchinjwa wakati mwanamke mwingine, Defroza Gedion (18) alipigwa hadi kupoteza maisha.
Mkoani Kilimanjaro, polisi wanamshikilia mfanyabiashara mmoja wa mjini Moshi kwa tuhuma za kumuua kikatili hawara yake.
Inasemekana kitendo hicho kilikuja baada ya mwanamke huyo kukataa kufanya naye ngono, akishinikiza kwanza apewe Sh 10, 000.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, jana alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa ambaye baada ya kumuua mpenzi wake, Sekunda Mushi (42), aliitupa maiti kwenye shimo la taka.
Huko Mbeya, Polisi mkoani humo, wanawasaka watu wawili wakazi wa vijiji cha Shoga na London, wilayani Chunya kwa tuhuma za mauaji ya wanawake wawili kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema matukio hayo yalitokea Februari 6 mwaka huu.
Msangi alisema mauaji ya mwanamke katika Kijiji cha Shoga, yamefanywa na mchimbaji wa madini.
Kuhusu mauaji yaliyotokea katika Kitongoji cha London, Kamanda huyo alisema mwanamke mmoja ameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo na mume wake
MWANANCHI.













No comments:
Post a Comment