Idara ya Uhamiaji nchini inatuhumiwa kuwatesa watu 41 wa familia moja akiwamo mzee mwenye umri wa miaka 88 ambao ni wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera, kwa kuwafungia kwa siku nne katika daraja linaloziunganisha Tanzania na Uganda kwa madai kwamba si raia.
Mzee Elika Tibahulira (88), mkewe, Mole Tibahulira (58), watoto wao na wajukuu, kwa pamoja walikamatwa usiku wa kuamkia Januari 22, mwaka huu katika Kijiji cha Murongo na kuamriwa waondoke nchini kwa maelezo kwamba siyo Watanzania.
Maofisa Uhamiaji wa Tanzania wanadaiwa kuwa waliwachukua kwa lengo la kuwakabidhi kwa maofisa wa Uganda, lakini habari zinasema maofisa wa nchi hiyo jirani walikataa kuwapokea wakisema kwamba hawawatambui.
Baada ya kufukuzwa Tanzania na kukataliwa Uganda, watu hao waliweka makazi kwenye eneo huru ambalo ni Daraja la Murongo juu ya Mto Kagera linaloziunganisha nchi hizo mbili na kukaa hapo kwa siku nne.Mmoja wa waathirika, George Ruteleza alisema Januari 26 mwaka huu, saa za asubuhi, maofisa uhamiaji waliwachukua kutoka darajani hapo hadi Kituo cha Polisi Murongo kuandikisha maelezo kisha kufikishwa mahakamani.
“Tulikaa hapo hadi jana (juzi, Januari 27, mwaka huu) saa moja usiku na watu wa uhamiaji wakatutoa polisi kwa maelezo kwamba wanakwenda kutupa maelekezo ya ziada, lakini waliturejesha tena mpakani na wakasema turudi kwetu,” alisema Ruteleza.
Mwathirika mwingine, Willibald Erika alisema: “Tulipofika mpakani tulikataa kuondoka maana tulishawaeleza kwamba sisi ni Watanzania. Walituacha kwa muda kama wa saa moja hivi na baadaye walirudi saa mbili hivi usiku na kuanza kutuchapa fimbo.”
Alisema walipigwa na kiasi cha kukimbilia vichakani kila mmoja kwa njia yake... “Leo asubuhi ndiyo tumeanza kutafutana na hadi sasa tupo 26, wenzetu 15 hatujui wako wapi.” Habari zinasema kuwa watu hao walipelekwa kituo cha polisi kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu.
Massawe jana alithibitisha habari hizo na kusema alielekeza wapelekwe polisi kisha mahakamani baada ya kuarifiwa kwamba walikuwa wakiendelea kuteseka kwa kukaa kwenye daraja.
“Kwa hiyo hayo ndiyo maelekezo niliyotoa na ninaamini yametekelezwa. Kama kuna mambo mengine yametokea huko nadhani wenye sheria kujua nani mhamiaji haramu na nani siyo ni uhamiaji wenyewe,” alisema.
Polisi na Uhamiaji
Ofisa Uhamiaji katika mpaka wa Murongo, Festus Sanga alikiri kukamatwa kwa watu hao akisema kuwa ni mwendelezo wa kuwaondoa wahamiaji haramu ambao walikwepa Operesheni Kimbunga.
“Kwa mujibu wa sheria za uhamiaji, mtu yeyote ambaye siyo raia wa Tanzania anapaswa kurudishwa kwao. Kwa hiyo sisi tulipowapeleka, kwa bahati mbaya ni kwamba maofisa wa Uganda walikataa kuwapokea na sisi ilibidi tuweke ulinzi upande wetu ili wasirudi,” alisema Sanga.
CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment