Wednesday, 29 January 2014

MDUNGUAJI AVAMIA TARIME NA KUUA WATU 9



JESHI la Polisi limeanzisha operesheni maalumu ya kumsaka mtu anayedaiwa kuwa jambazi, ambaye anaendelea kufanya mauaji wilayani Tarime.
Jambazi huyo ambaye amefanya mauaji katika vijiji vya Mogabiri na Nkende, wilayani Rorya Tarime, imeelezwa mpaka sasa ameshaua watu tisa na kujeruhi wengine wawili, ambapo anatembea na bunduki aina ya SMG.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi nchini, Paul Chagonja alisema, muuaji huyo amekuwa akiua watu wasio na hatia, pia inasadikiwa kuwa si mkazi wa eneo hilo bali ni mgeni.


Alisema sababu ya mtu huyo kufanya mauaji hayo haijulikani kwani anapofanya mauaji hachukui mali isipokuwa vitu vidogo, ambapo alisema anachukua simu, mikate, biskuti na soda.
“Januari 26, saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mogabiri katika Mkoa wa kipolisi Tarime Rorya, alimwua kwa risasi Zakaria Marwa (28) na Erick Lucas (24) baada ya kukutana nao njiani,” alisema Chagonja.
Alisema siku hiyo hiyo saa 4 usiku katika kijiji hicho alimwua Robert Kisiri (45) baada ya kuvamia baa inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine. Aliongeza kuwa siku iliyofuata saa 11.30 alfajiri alifanya mauaji mengine katika kijiji hicho kwa kumpiga risasi David Matiko (39) na kumpora simu aina ya Nokia.
Katika tukio hilo, alimjeruhi Machungu Nyamahemba (19) ambaye bado amelazwa Hospitali ya Tarime kwa matibabu. Chagonja aliongeza kuwa siku hiyo saa 2 usiku katika kijiji cha Nkende alimwua Juma Nyaitara (30) na baada ya mauaji hayo alipora simu za mkononi za Chacha Magige na Masero Marigiri. “Usiku wa kuamkia Januari 28, aliua watu wengine watatu ambao bado majina yao hayajafahamika.
Mmoja alipigwa risasi wakati akiendesha pikipiki katika kijiji cha Nkende, wengine wawili waliuawa baada ya kukutwa wakitengeneza gari lililokuwa limewaharibikia katika kijiji cha Mogabiri,” aliongeza.
Mpaka sasa juhudi za kumsaka mtu huyo bado zinaendelea, pia wanashirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kufanikisha kukamatwa kwa mtu huyo.
Alisema Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu ametuma timu maalumu kutoka makao makuu ya Polisi inayohusisha Kamisheni ya Operesheni, Upelelezi na Intelijensia kwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na ngazi ya mkoa, kuhakikisha mtu huyo anakamatwa haraka iwezekanavyo ili kuwaondoa hofu wananchi.
“Anaua watu wasio na hatia na sababu ya kufanya mauaji hayo haijulikani kwa sababu hakuna mali anazochukua, lakini tutahakikisha jambazi huyu anapatikana ili wananchi waendelee kuishi kwa amani,” alisema.
Chagonja alisema wanatoa mwito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano ili mtu huyo aweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria haraka, alitaka kwa yeyote atakayekuwa na taarifa atumie namba maalumu ambazo ni 0754 785 557.
Taarifa za awali Taarifa zilizopatikana mapema, zilisema watu waliopoteza maisha walitambuliwa kuwa ni askari mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Zakaria Mwita ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa na aliyekuwa Mhandisi Ujenzi wa Wilaya ya Rorya na Mkandarasi, David Misiwa ambaye pia alikuwa akimiliki kampuni binafsi ya Yomani.
Wengine waliouawa katika mashambulizi tofauti ya siku tatu kuanzia Januari 26 hadi juzi, ni aliyekuwa mfanyabiashara wa magari ya kusafirisha abiria, Samwel Mohenga na mwendesha bodaboda mkazi wa kijiji cha Nkende, Juma Nyaitara.
Wengine ni Erick Makanya ambaye ni mjukuu wa Meja Jenerali Marwa na mfanyabiashara wa duka la nyama mkazi wa kijiji cha Rebu, Juma Mroni na mkazi wa Kenyamanyori, Robert Kisiri. Kutokana na hali hiyo, jana kati ya saa 4 na 5 asubuhi mtu aliyekuwa amevaa koti refu alinusurika kushambuliwa na wananchi akidhaniwa ndiye muuaji anayesakwa, lakini aliokolewa na polisi waliolazimika kufyatua risasi angani na kutawanya wananchi hao na kisha kumpeleka kituoni.
Ilibainika hakuwa anayesakwa. Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime, jana walitembelea maeneo ya mauaji hayo.
Adaiwa kuua hawara Mkazi wa kijiji cha Kisa, tarafa ya Kipeta, bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga , Josephat Chinga ‘Bonge’ (32) anadaiwa kumwua hawara wake kikatili kwa kumchinja kisha kuhifadhi kichwa chake ndani ya sufuria.
Pia anatuhumiwa kukata viganja vya mwanamke huyo na kutokomea navyo kwa imani za kishirikiana. Inadaiwa Chinga alikodisha watu wanne kumwua hawara huyo kwa ahadi ya malipo ya Sh milioni 1.6 - ambapo kila mmoja angelipwa Sh 400,000 - baada ya mauaji hayo.
Taarifa kutoka eneo la tukio ambazo zilithibitishwa na Polisi zilidai kuwa Chinga alihitaji viganja vya mpenzi wake huyo, kwa kuwa vina alama ya ‘M’ ambayo ni imani kuwa alama hiyo inahitajika kutengeneza dawa ya kutajirisha mtu.
Mtoa taarifa kutoka eneo la tukio, alidai kuwa baada ya Chinga kushindwa kutimiza ahadi yake ya uwalipa kiasi hicho cha fedha, watuhumiwa hao waliokodishwa walimwibia kichwa alichokuwa amehifadhi kwenye sufuria na kukitelekeza kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi ya Kisa.
Inadaiwa watuhumiwa hao waliandika barua na kueleza mkasa mzima kisha kuipachika pembeni mwa sufuria lenye kichwa cha marehemu. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alibainisha kuwa watuhumiwa hao walikamatwa mwanzoni mwa wiki hii, baada ya kichwa hicho kugundulika kwenye uwanja wa michezo.
Mwaruanda aliongeza kuwa mwanamke huyo, Ritha Malecela (35) alipotea katika mazingira ya kutatanisha Desemba mwaka jana hadi mwanzoni mwa wiki hii.
Uchunguzi wa awali kwa mujibu wa Mwaruanda ulibainisha kuwa Desemba 10, mwaka jana Ritha ambaye alikuwa akiishi kinyumba na Chinga baada ya kutoroka kwa mumewe na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Polisi kwa kushirikiana na wananchi tuliendesha msako bila mafanikio wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu kupotea kwake, Januari 23 kichwa cha mwanamke kilikutwa katika uwanja wa michezo kwenye sufuria,” alibainisha.
Mwaruanda alibainisha kuwa pembeni mwa sufuria hilo kulikuwa na barua inayosadikiwa kuandikwa na mmoja wa watuhumiwa hao, akimtaja Chinga aliyekuwa hawara wa marehemu ndiye aliyewakodisha kumwua Ritha.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda baada ya kufanya mauaji hayo walitupa ndani ya Ziwa Rukwa huku kichwa chake kilichukuliwa na hawara yake ambaye aliwaahidi ujira wa Sh 400,000 - kila mmoja aliyeshiriki kumwua mwanamke huyo .
Inadaiwa kuwa baada ya Chinga kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuwalipa ‘wauaji ‘ hao mmoja wao aliamua kutoboa siri hiyo hadharani. Kamanda Mwaruanda akifafanua alidai kuwa watuhumiwa wanne walikamatwa ambao ni pamoja na ‘hawara’ wa marehemu, wengine ni Joseph Milumba (31), Geofrey Ndenje (27) na Grace Sindani (40) ambaye inasemekana alimrubuni na kumtorosha Ritha kutoka kwa mumewe na kumpeleka kwa Chinga kwa lengo la kumwua.
Inadaiwa mtuhumiwa mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja anatafutwa na Polisi baada ya kutoroka na kujificha kusikojulikana mara baada ya kufanyika mauaji hayo.
Kamanda Mwaruanda alidai kuwa bado jitihada za kukitafuta kiwiliwili cha marehemu katika Ziwa Rukwa zinaendelea ambapo watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lao kukamilika .
Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime, Petty Siyame, Sumbawanga na Katuma Masamba, Dar

CHANZO HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!