Saturday 25 January 2014

NIMEJENGA NASOMESHA KWA KAZI YA KUKAANGA SAMAKI FERI...

 Dotto akiwa katika shughuli zake za kukaanga samaki


Ni eneo ambalo limetanda moshi mzito ukiambatana na moshi wa sigara, kutoka kwa baadhi ya wanaofanya kazi kwenye eneo hilo.
Napata shauku ya kufahamu ni kwa namna gani binadamu anaweza kukaa kwenye moshi kama huo, anapata nini hadi anahamasika kukaa humo.

Nazidi kusogea na kugundua kuwa licha ya kuwapo kwa watu wachache wanaovuta sigara, pia kuna wanaume wanaofanya kazi huku wakinywa pombe ya viroba na waliotulia wakifanya kazi moja tu ambayo imewafanya wawe hapo; ya kukaanga samaki.
Tofauti na tulivyozoea, jiko hilo lina wakaanga samaki wasiopungua 30, wote wakiwa ni wanaume watupu.  Hapa siyo pengine bali ni katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, lililopo jijini Dar es Salaam.
Nasogea na kukutana na kijana ambaye ni miongoni mwa wale ambao hawana sigara mdomoni, anaonekana tofauti na walivyo wengine kwa kuwa yeye ni msafi na yuko makini.
Ninaanza mazungumzo na yeye;

Swali: Umefanya kazi hii kwa miaka mingapi?

“Huu ni mwaka wa 10, tangu nianze kufanya kazi hii, nina familia na ninasomesha watoto wangu wawili bila shida,” ananijibu Sebastian Lukas, maarufu kwa jina la  Dotto.
Ananieleza ni kwa nini anaitwa Dotto badala ya Sebastian, anasema ni kutokana na kufanana sana na kaka yake ambaye naye ni mkaanga samaki kiasi hata mama yao mzazi huwa hawezi kuwatofautisha. “Huyu kaka yangu hatukuzaliwa mapacha bali watu walivyoona tumefanana wakaanza kuniita Dotto hadi leo jina hilo limekua.”
Dotto alizaliwa mwaka 1982, katika Kijiji cha Itundwi kilichopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma na kupata elimu ya msingi kwenye Shule ya Chungai hapo hapo kijijini.

Anasema kuwa baada ya kumaliza elimu ya msingi alichaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza katika Shule ya Pai na kusoma hadi kidato cha pili, lakini kutokana na sababu mbalimbali alishindwa kuendelea na masomo yake.
Dotto anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na mfumo wa ufundishaji uliokuwa ukitumika shuleni hapo, ambapo walimu walikuwa hawaingii darasani na wakiingia hawafundishi mpaka mwisho.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!