Friday 24 January 2014

MAWAZIRI WA FEDHA WA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR WAKUBALIANA KUONGEZA USHIRIKIANO KATIKA UTENDAJI WA KAZI

DSC_0004Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya akiwa pamoja na Waziri wa Fedha wa Zanzibar Omar Yussuf Mzee wakiingia katika Ukumbi wa Mkutano huko katika Hoteli ya Serena Inn Shangani Mjini Zani
NA RAMADHAN ALI/MAELEZO ZANZIBAR 

Mawaziri wa Fedha wa Tanzania Bara, Sada Salum Mkuya na Waziri mwenzake wa Zanzibar Omar Yussuf Mzee wamekubaliana kuongeza ushirikiano  katika utendaji wa kazi ili kuona pande zote mbili za Muungano  zinapiga hatua katika maendeleo .
Wakizungumza katika mkutano  wa kwanza  wa kujuana baada ya Rais Kikwete  kumteua Sada Salum Mkuya kuongoza Wizara ya Fedha ya Tanzania Bara, Mawaziri hao  wameamua kukutana mara kwa mara ili kupunguza changamoto zinazozikabili Wizara hizo.
Katika hatua ya awali ya ushirikiano, Waziri wa Fedha wa Zanzibar Omar  Yussuf Mzee amemueleza Waziri wa Fedha wa Tanzania Bara kwamba wanajukumu kubwa kuona Tume ya Fedha ya pamoja inafanyakazi.
Akizungumzia misaada ya wafadhi ambao hivi sasa wameielekeza  zaidi kwenye  sekta, Waziri Omar Yussuf ametaka pande zote mbili za Muungano zishirikiane na ionekane kuna gao la sekta husika kwa upande wa Zanzibar.
“Wafadhili hivi sasa wanapenda kusaidia sekta, naomba tusimamie kuona sekta husika za pande zote mbili zinafaidika na msaada huo, ” alisisitiza Waziri wa Fedha wa Zanzibar.
Waziri Omar Yussuf Mzee amemuahidi Waziri Mkuya kwamba atampa kila ushirikiano na kufanya kazi naye kwa karibu  kama alivyokuwa akifanya kwa Waziri aliepita Marehemu William Mgimwa.
Kwa upande wake Waziri Sada Salum Mkuya amesema ameamua kutoa kipaumbele kwa Zanzibar katika kuanza majukumu yake kwa sababu Wizara hizo mbili za Fedha ni muhimu sana katika kukuza na kuimarisha uchumi.
Amekubaliana na wazo la Waziri mwenzake wa Zanzibar la kukutana mara kwa mara kwani anaamini  kwamba kero nyingi za muungano zinaweza kupatiwa ufumbuzi  ndani ya vikao hivyo.
“Mambo mengi ya Muungano yalikuwa hayapatiwi ufumbuzi kwa sababu hatukutani, naahidi tutakutana mara kwa mara ikiwa  Zanzibar, Tanzania Bara ama sehemu nyengine yeyote, ”alisema Waziri Sada Salum Mkuya.
Ameahidi atahakikisha kwamba masuala ya Kimataifa katika Wizara za Fedha, nafasi ya Zanzibar  inakuwepo wakati wote ili kuhakikisha  tija inapatikana kwa pande zote.
Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena Inn Shangani Mjini Zanzibar uliwashirikisha Manaibu Mawaziri wa Fedha wa Tanzania Bara Adam Kigoma Malima na Mwigulu Lameck Mchemba pamoja na viongozi wa wengine wa ngazi za juu wa Wizara hizo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!