WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesisitiza wafanyabiashara kununua mashine za kutolea stakabadhi za ununuzi zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuwezesha Serikali kupata fedha zinazotokana na kodi zinazokusanywa. Alisema hayo jana wakati akizindua mradi wa maji katika Shule ya Msingi Olomitu, iliyoko Kata ya Mlangarini wilayani Arumeru. Mradi huo umefadhiliwa na Kampuni ya maua ya Kiliflora.
Waziri Mkuu alisema mashine hizo ni za uhakika na hazina tatizo na zinauzwa Sh 800,000 lakini baada ya wafanyabiashara hao kulalamika bei kubwa TRA ilipunguza bei hadi Sh 600,000. Aliongeza kuwa wazabuni walijitokeza kuomba zabuni za uuzaji wa mashine hizo, lakini 11 ndio walipitishwa na TRA kuziagiza na kuuzia wafanyabiashara nchini.
Alihoji, “ ufisadi uko wapi wakati kampuni 11 ziliteuliwa kuuza mashine hizo? Pia mkumbuke kuwa gharama za ununuzi wa mashine hizo mtarudishiwa kadri mnavyokusanya mapato na kuisaidia Serikali.
“Hakuna sababu ya kuona jambo hili kama kero bali ni elimu tu kwa maana mnaponunua mashine hizo mnarudishiwa fedha zenu, hivyo nakuombeni wafanyabiashara muachane na masuala ya kudai kuwa kuna ufisadi, hapana,” alisema.
Aliendelea:“Elimu itolewe zaidi ili watu wajue faida za mashine hizi, pia Serikali itaendelea kuhakikisha maji yanapatikana kwa wingi ili kupunguzia wanawake kero ya kutembea umbali mrefu kufuata maji”.
Mgomo usitishwe Katika hatua nyingine, Serikali imebaini kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa kuchochea mgogoro huo kwa kuwa hawataki kulipa kodi. Sambamba na hilo, Serikali imetaka wafanyabiashara hao kusitisha mgomo wao na kuendelea kulipa kodi kwa sababu ni wajibu wa kila mtu.
Aidha, Serikali imesema malalamiko ya wafanyabiashara hao kuhusu bei ya mashine za kutolea stakabadhi EFDs yanajadilika na kwa sasa iko katika majadiliano na msambazaji wa mashine hizo kwa ajili ya kuhakikisha zinashuka bei zaidi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wa mashine hizo na pia kutoa majibu ya malalamiko ya wafanyabiashara, baada ya mgomo wa karibu siku mbili, Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Saada Salum Mkuya na Janeth Mbene walisema Serikali inataka watu wanaochochea mgomo huo waache.
Juzi na jana mamia ya wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma kufungua maduka na kusababisha shughuli zote za biashara kusimama wakipinga matumizi ya mashine, hatua hiyo mbali na kusababisha adha kwa wananchi wa ndani na nje ya Jiji na nchi jirani waliofika kununua bidhaa.
Akitoa ufafanuzi, Mkuya alisema mashine za EFDs zinatumiwa kwa wafanyabiashara ambao mauzo yao ni kuanzia Sh milioni 14 hadi Sh milioni 40 kwa mwezi, lakini wafanyabiashara wanaogoma Kariakoo wengi wao ni wafanyabiashara ambao hawahusiki na mashine hizo.
“Kuna wafanyabiashara wachache tu wanachochea mgomo huu, kwa sababu tu hawataki kulipa kodi wakati wakijua wafanyabiashara wengine hawahusiki na mashine hizo, lakini wakitaka kufungua maduka yao wanaambiwa yatachomwa moto, huu ni ukiukwaji wa sheria zaidi,” alisema Mkuya.
Alisema mfumo wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza awamu ya kwanza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na awamu ya pili ni hii ya mwaka huu, ikihusu wafanyabiashara ambao hawakusajiliwa kwenye VAT ambao mauzo yao ghafi kwa mwezi ni Sh milioni 14 hadi 40.
“Ikumbukwe kuwa gharama zote za ununuzi wa mashine hizi zitarudishwa kwa mfanyabiashara atakapowasilisha mahesabu yake ya kodi atasamehewa pindi atakapowasilisha mahesabu yake, hivyo itafanya Serikali kulipia gharama za mashine kupitia kodi,” alisema.
Alisema malalamiko kuwa mashine hizo zinapatikana kwa bei nafuu Dubai na China, kuwa taarifa hizo si sahihi na kwamba mashine hizo zilitengenezwa maalumu kwa ajili ya matumizi ya Tanzania kulingana na mahitaji haziwezi kufanana. Naibu Waziri huyo alisema kumekuwa na malalamiko kuwa utumiaji wa mashine utasababisha wafanyabiashara kutozwa kodi ya VAT ya asilimia 18, alisema ukweli ni kwamba awamu hii ya pili hawakati bali ni kwa ajili ya kodi ya mapato.
Alisema wafanyabiashara zisizo rasmi aina ya mama lishe, wamachinga na wengine ambao hawana sehemu maalumu ya kufanyia biashara na wasiofikia mauzo ya Sh milioni 14 hawahusiki katika mashine hizo hivyo waendelee na shughuli zao.
Wanaolengwa ni wenye maduka makubwa ya spea, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na spea zake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, wauza pikipiki na biashara nyingine.
“Kwa nchi nzima tumelenga wafanyabiashara 200,000 tu kwa awamu hii ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na nusu waliosajiliwa kulipa kodi,” alisema.
Alisema tuhuma kwamba mfumo wa EFD ni mradi wa mtu, tuhuma hizo si za kweli, kwa sababu mchakato wa ununuzi wa mashine ulifanyika kwa wazi kupitia zabuni ya kimataifa na kupatikana wasambazaji 11 na watengenezaji mashine.
Alisema TRA pamoja na wasambazaji na watengenezaji walifikia mwafaka, kwamba bei za mashine ziuzwe kuanzia Sh 600,000 na bei kikomo ni Sh 778,377 bei ambayo ni nafuu ikilinganishwa na nchi zingine zinazotumia mashine hizo.














No comments:
Post a Comment