Tuesday, 29 October 2013

WATU WAZIMIA WAKATI KESI YA MAUAJI YA ERASTO MSUYA IKIPIGWA KALENDA HADI DEC 11



Ndugu wa Marehemu ERasto Msuya waliofika Mahakamani wakimuondoa Mdogo wa Marehemu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kumuwaisha Hospitali baada ya Kupoteza Fahamu muda mfupi tu baada ya Mahaka ya Hakimu Mkazi Moshi, kuahirisha Kesi hiyo hadi Desemba 11.


Mshitakiwa namba mbili, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), anayetuhumiwa na wengine saba, kumuua Mfanyabiashara Erasto Msuya kwa kumpiga risasi akitoka kwa taabu nje ya mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Desemba 11, mwaka huu




Washtakiwa namba 8, Ally Mussa "Majeshi" (aliyevaa suruali ya bluu) na mwenzake wakifunika nyuso zao kukwepa Kamera ya Mpiga picha wetu, wakati wakiondolewa Mahakamani, muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11, mwaka huu.


Mshitakiwa, Sharif Mohamed Athuman (31), ambaye ni mshitakiwa namba moja katika kesi ya Mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite, Erasto Msuya mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, muda mfupi baada ya  kesi hiyo kuahirishwa hadi Desemba 11, mwaka huu.





Washitakiwa Joseph Damian "Chusa" na mwenzake Shaibu Jumanne Saidi "Mredi", wakimsaidia Mshitakiwa mwenzao kupanda katika Gari la Polisi muda mfupi baada ya kesi inayowakabili ya mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite, Erasto Msuya kuahirishwa hadi Desemba 11, mwaka huu







MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Moshi,  imeahirisha Kesi ya Mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite Jijini Arusha,Erasto Msuya (43), hadi Desemba 11 mwaka huu.  


Kesi hiyo iliyotajwa katika Mahakama hiyo kwa mara kwanza, Agosti 21, mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi, Munga Sabuni, inawakabili watuhumiwa 8 wanaodaiwa kuuwa kwa kukusudia kinyume cha Sheria ya Makosa ya jinai, Kanuni ya 16, Kifungu cha 196.


Pamoja na idadi ya Watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na Mauaji hayo ya kikatili, yaliyotokea Agosti 7, katika maeneo ya Mjohoroni, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kukamilika, Upande wa Mashtaka, ukiongozwa na Wakili, Janet Sekule, uliwasilisha Maombi ya kutaka Kesi hiyo ipangiwe Tarehe mpya ili kupisha Upepelezi kukamilika.


Wakili Sekule, alisema kuwa kutokana na uzito wa Kesi hiyo, Jamhuri ingependa kupatiwa muda wa kukusanya ushahidi wa kutosha ambao utawasaidia katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupata pingamizi lolote kutoka upande wa Washtakiwa.


 “Mheshimiwa Hakimu, kutokana na uzito wa shauri la kuuwa kwa makusudi kinyume na kanuni namba 16, kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya jinai, inayowakabili washtakiwa namba 1 hadi 8, Jamhuri inaiomba Mahakam yako tukufu, kupewa muda wa kukamilisha ushahidi,” alisema Sekule.


Baada ya kuridhika na maelezo ya Maombi ya Upande wa Jamhuri, Mahakama ya Hakimu Mkazi Munga Sabuni, iliahirisha Kesi hiyo hadi Desemba 11, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.


Katika Kesi hiyo, Mshtakiwa namba Tano, Joseph Damas Mwakipesile “Chusa” (36), ambaye ni Mfanyabiashara Maarufu wa Madini anadaiwa kuwa alishirikiana na Mshtakiwa Ally Mussa “Majeshi”, anayedaiwa kuwahi kulitumikia Jeshi la kujenga Taifa (JKT), kabla ya kufukuzwa pamoja na wengine 6 kumuua kwa kumpiga Risasi 13, Bilionea wa Madini, Erasto Msuya (43).


Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa mnamo, Agosti 7, mwaka huu majira ya6:30 mchana walifanya kitendo hicho  kando ya barabara kuu ya Arusha– Moshi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Washtakiwa wengine ni, Sharif Mohamed Athuman (31), mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir ‘Msudani’ au ‘Mnubi’(32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata wilayani Hai, Karim Kihundwa (33) mkazi wa Kijiji cha Lawate Wilaya ya Siha na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.


Credit: Taifa Letu

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!