Viongozi wa dini wametaja majina 61 ya vinara wanaojihusisha na dawa za kulevya nchini ambao wanatarajia kuwaburuza katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mjini The Hague, Uholanzi kujibu tuhuma zao.
Majina hayo yametajwa na Kamati ya Maadili na Haki za Jamii kwa Viongozi wa Dini na Wananchi nchini, ambapo miongoni mwao wamo wabunge wa majimbo na viti maalum, mawaziri, viongozi wa dini na wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipendekoste, William Mwamalanga, aliliambia gazeti la Nipashe kuwa, majina hayo yalipatikana Jumanne wiki hii kupitia mkutano wa siri wa viongozi wa dini wa madhehebu ya kiislam na kikristo 134 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Pemba.
Mkutano huo ambao ulifanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 21, mwaka huu hapa jijini Dar es Salaam uliwakilishwa na viongozi wawili wa dini kila mkoa isipokuwa Rukwa ambapo hapakuwa na mwakilishi.
Alisema ulifanyika kwa siri ili kutotoa mwanya wa kuingiliwa na mifumo isiyo rasmi ambayo ingevuruga adhima yao.
Kuhusu upatikanaji wa majina, mchungaji huyo alisema ulitokana na utafiti walioufanya ndani na nje ya nchi.
Pia alisema taarifa nyingine walizipata kupitia kwa wasiri wao kutoka ndani ya jeshi la polisi nchini na vyanzo mbalimbali vya habari kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia mkutano huo, alisema lengo lake lilikuwa ni kutathmini biashara za dawa hizo ambazo alieleza ni tishio linaloangamiza kwa kasi kubwa vijana na kusababisha nchi kuingia kwenye aibu duniani.
Mchungaji Mwamalanga alisema katika mkutano huo walitoka na maazimio mawili likiwamo la kuwafikisha mahakamani wahusika na kufanya kampeni za siri kupita kwenye majimbo sita ya wabunge (majina tunayo) waliotajwa.
Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwaeleza wananchi tabia za wawakilishi wao ili mwaka 2015 waweze kuchagua viongozi bora wenye uchungu na nchi yao, wakereketwa wa amani na watakaochochea watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Alisema wakati wa uchaguzi mkuu wawakilishi wa mkutano huo, watapita tena majimboni kuwataja wahusika kwa majina.
Kuhusu viongozi wa dini ambao nao wametajwa kujihusisha na biashara hiyo, mwenyekiti huyo alisema, mkutano umewataka wafuate mfano wa Mchungaji Donald Mwakisambwe wa kanisa la Kiinjili la Kipentekoste nchini, ambaye aliacha kwa ridhaa yake.
Aidha, kamati hiyo imetoa siku 71 kuanzia Jumanne ya wiki hii kwa wahusika wote 61 kujisalimisha wenyewe kwa Rais Jakaya Kikwete.
“Wakati mchakato wa kuyapeleka majina haya ICC ukiendelea tunawataka wahusika wajisalimishe kwa Kikwete kwa kuwa orodha hii tuliyonayo (akitaja majina yao) ni miongoni mwa wale waliotajwa kwenye orodha aliyokabidhiwa Rais wakati ule, wakijisalimisha tutajua kupitia wasiri wetu,” alisema na kuongeza:
“Vinara hawa ambao Watanzania wamekuwa wakiwaita ‘vigogo wa dawa za kulevya’ hawapaswi kuitwa jina hili, hawa ni wahuni na wauaji, tusiwape majina mazuri ambayo yanawatukuza ndiyo maana biashara hii inakuwa kwa kasi,” alisema.
Kuhusu Watanzania 175 waliokamatwa nchini China ambao wanasubiri adhabu ya kunyongwa na wengine waliowahi kukamatwa nchi nyingine duniani alisema, utafiti waliofanya unaonyesha kuwa wengi wao hutumwa na wakubwa hapa nchini na kuahidiwa fedha nyingi.
“Tumekubaliana wakati vijana wetu wakisubiri adhabu hiyo ya kunyongwa basi ICC iwatambue wahuni (vigogo) wanaosababisha biashara hii hapa Tanzania,” alisema.
Alisema katika mkutano huo wa siri alikuwapo mtaalam wa sheria mstaafu aliyekuwa akifanya kazi katika mahakama ya ICC ambaye amewasaidia jinsi ya kufungua kesi hiyo mahakamani hapo.
Aliongeza kuwa, kesi hiyo itaambatanishwa kielelezo cha asadi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambayo aliitoa mwezi Agosti mwaka huu bungeni kwa kusema kuwa hawezi kuwataja hadharani wabunge waliotajwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Katika taarifa ya waziri Lukuvi alisema serikali haiwezi kuwataja kwa haraka kwa kuwa haina ushahidi kwa kuhofia kushindwa mahakamani.
Mchungaji Mwamalanga alisema maelezo ya Lukuvi kwao ni ushahidi kuwa, wapo wanaojihusisha na biashara hizo.
Akibainisha miongoni mwa tafiti walizowahi kufanya katika majimbo nane nchini ambayo ni Dar es Salaam (Kinondoni), Tanga, Mbeya, Mwanza, Iringa , Dodoma, Lindi, Arusha alisema kila wiki kati ya vijana watano hadi sita hupoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Alisema wilaya ya Kinondoni walibaini tatizo ni kubwa ambapo ni mara tatu ya idadi hizo hapo huu.
“Utafiti ulibaini asilimia kubwa ya waendesha bodaboda wamekuwa wakifariki na vyombo vyao kutokana na kujihusisha na matumizi ya dawa hizi, ukubwa wa tatizo ulionekana kwenye mikoa ya Tanga, Mbeya na Dar es Salaam,” alisema.
Mwenyekiti huyo, alisema mkutano huo umemtaja Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kuwa ni waziri aliyefanya vizuri katika mapambano hayo ambaye amesababisha kwa sasa usafirishwaji wa dawa hizo kwa njia ya viwanja vya ndege kukoma.
Pia alisema Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzoa, amejitahidi kupambana na tatizo hilo kwa kuwa muwazi na mwaminifu (kutopokea rushwa).
Katika hatua nyingine, gazeti la NIPASHE limechukua nafasi ya kwanza katika kuibua na kuzichapisha habari mbalimbali zinazohusu dawa za kulevya na kusababisha baadhi ya wauzaji kujisalimisha wenyewe.
Mchungaji Mwamalanga alisema nafasi hiyo imekuja kupitia utafiti wao uliohusisha gazeti tofauti nchini ambapo NIPASHE liliibuka kidedea baada ya kuonekana mara kwa mara ikitoa taarifa za dawa za kulevya.
“Katika mkutano wageni wetu kutoka nchi ya Kidemokrasia ya Kongo, walieleza jinsi NIPASHE lilivyosaidia viongozi wao wa dini 14 waliokuwa wakijuhusisha na biashara hiyo, walivyoacha baada ya gazeti hili kuibua habari mbalimbali,” alisema.
Katika hatua nyingine, mkutano huo, umempongeza Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, kufuatia hatua yake ya kusimama kuwatetea wazawa na kuhakikisha kuanzia sasa wataanza kumiliki na kunufaika na maliasili zao.
Alisema Dk. Mengi amekuwa kiranja wa Watanzania kuhusu gesi na ameifanya serikali kuwa sikivu na kuruhusu wazawa sasa kuwekeza kwenye hilo na maliasili nyingine.
Alisema kamati yao inaungana na Dk. Mengi na kusema gesi isiwe laana bali iongeze upendano na isitumiwe na wanasiasa wachache kuchafua amani.
Pia alisema sheria na sera ya gesi inayoandaliwa hivi sasa itasaidia kulilinda Taifa.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment