Friday 18 October 2013

UTATA WAGUBIKA UJIO WA ALEX MASSAWE


HATUA za kumrejesha nchini mfanyabiashara maarufu, Alex Massawe, aliyefikishwa mahakamani nchini Dubai Falme za Kiarabu (UAE) kwa tuhuma za mauaji, zimegubikwa na utata mkubwa, huku Tanzania ikidaiwa kushindwa kutimiza masharti ya Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol).
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka Dubai, Interpol iliipa Tanzania hadi kufikia Septemba 4, mwaka huu, iwe imewasilisha vielelezo vya kuthibitisha tuhuma zake.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa muda huo umemalizika bila Tanzania kuwasilisha uthibitisho huo na kwamba Massawe ameachiwa huru nchini humo.
Massawe alikamatwa Dubai kati ya Juni 20 na 25. Kwa mujibu wa Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Gustav Babile, ombi la kumleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi extradition request) lina hatua ndefu.
Alisema kuwa kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili Massawe aletwe, akasisitiza kuwa ilikuwa ni lazima kwanza Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe.
Jeshi la Polisi nchini limekanusha taarifa hizo za kuachiwa kwa Massawe, likisema halina taarifa za suala hilo, na kwamba taratibu za kisheria zinaendelea kufanyika.
Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alisema: “Mambo ya kusikia sisi hatuyafanyii kazi, kwanza vyanzo vingine vya habari ni vya kutiliwa shaka. Sisi tukijiridhisha tukawa na taarifa kamili tutawaambia.”
Naye Mkuu wa Interpol Tanzania, Babile, alisema kuwa Jeshi la Polisi limeshafanya taratibu zote za kiuchunguzi, limepeleka jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi.
Babile alisema kiutaratibu Jeshi la Polisi linapomaliza uchunguzi na kuandikia, kinachofuata ni jalada kupelekwa kwa DPP, ambaye akishajiridhisha hulipeleka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili taratibu za kuanza kumrejesha mtuhumiwa nchini ziweze kufanyika.
Hata hivyo taarifa ya awali iliyotolewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, baada ya kukamatwa Massawe, ilisema kuwa sheria inasema mtu akikamatwa nchi nyingine, anashtakiwa nchini humo, huku taratibu za kisheria za kumrejesha zikiendelea kwa nchi ambazo zina utaratibu wa kubadilishana wafungwa kama ilivyo Tanzania na UAE.
Taarifa za kukamatwa Massawe nchini Dubai zilipatikana Julai 11, mwaka huu, na kuthibitishwa na Babile, aliyesema mtuhumiwa huyo alikamatwa kati ya Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Aprili 4, mwaka huu, Massawe alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara, Onesphory Kituly, ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam
Katika kesi hiyo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa mwingine ni Makongoro Joseph Nyerere
chanzo:daima

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!