Mdogo wake mwandishi wa habari wa ITV/Radio One Ufoo Saro aliyejitambulisha kwa jina la Goodluck ameelezea jinsi ambavyo tukio lilotokea nyumbani kwao jana majira ya saa moja na nusu asubuhi ambapo shemeji yake Anthery Mushi alimpiga risasi dada yake na kumjeruhi tumboni na begani, na kumuua mama yake (mama mkwe) na kisha yeye mwenyewe kujiua kwa kujipiga risasi.
“Tulisikia sauti ya risasi sebuleni…na hapo mama akawa anatuita anasema njooni hapa nakufa, tulipotoka nje tukakuta na dada nae ndo yuko chini, akatuambia rudini ndani anataka kutuua wote hawa, ndo tukarudi ndani. Baada ya kurudi ndani ndo akaanza kupiga risasi milangoni na madirishani akawa anasema tokeni nje nataka niwauwe.” Alisema Goodluck.
“Baada ya polisi kuja na kuzunguka nyumba tukakuta mtu mwenyewe amekaa kwenye kochi na yeye kajiripua risasi. Tukaulizia dada yuko wapi tukaambiwa wamemuona dada mmoja hapa amechafuka damu amepelekwa Tumbi na pikipiki, ndo baada ya kufuatilia ndo tunasikia amepelekwa Muhimbili.”
Ufoo Saro amelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili na tayari amefanyiwa upasuaji. Jana kamishina msaidizi wa upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam Hemed Msangi,amesema kuwa Ufoo amejeruhiwa eneo la mkononi, begani na tumboni na hali yake inaendelea vizuri.
Chanzo: Taarifa ya habari 100.5 Times fm














No comments:
Post a Comment